Mgogoro kufunga Bunge la EALA
Bunge la jumuiya ya Afrika mashariki
huenda likafungwa iwapo baadhi ya viongozi wakuu wa Afrika mashariki
hawataingilia kati kufuatia migogoro ya takriban miezi sita sasa
inayolikumba.
Hali hiyo inatokana na kwamba mataifa yaliowachagua
viongozi hao kama wawakilishi wake hayana uwezo wa kuwaadhibu wabunge
hao kulingana na Gazeti la jumamosi la The Citizen nchini Tanzania.Bunge la Tanzania limekiri kwamba halina uwezo wa kuwasimamisha kazi wawakilishi wake katika bunge hilo ,licha ya kwamba wanaendelea kuzozana.
Hatua hiyo inajiri baada ya chama cha FDC nchini Uganda kulitaka bunge la nchi hiyo kuwafuta kazi wawakilishi wake kwa kuwa wabunge hao hawatekelezi wajibu wao.
Bunge la EALA limeshindwa kufanya kazi katika miezi iliopita huku wanachama wakiwa na mpango wa kumuondoa Spika wa bunge hilo Maregeret Zziwa kwa madai kwamba ameshindwa kutekeleza wajibu wake inavyohitajika.
Kulingana na The Citizen, katika wiki za hivi majuzi ,wanachama wa bunge hilo wameshindwa kufanya kazi zao mjini Kigali na baadaye Nairobi kufuatia mvutano kuhusu madai ya utovu wa nidhamu dhidi ya mwakilishi mmoja kutoka Tanzania ambaye wabunge wanataka aondolewe.
Wanaharakati katika eneo la Afrika mashariki wamelalamika kwamba mgogoro huo unazuia maendeleo ya eneo hili.
Maoni
Chapisha Maoni