Marekani yaidhinisha matumizi makubwa kwa ajili ya ulinzi
Baraza la seneti la Marekani limeidhinisha zaidi ya dola nusu trilioni kwa matumizi ya kijeshi siku ya Ijumaa. (12.12.2014) Mabilioni kadhaa ya fedha hizo zimetengwa makhususi kupambana na kundi la Dola la Kiislamu, IS.
Bunge la Marekani liliidhinisha muswada wa sheria kuhusu matumizi makubwa ya ulinzi siku ya Ijumaa yanojumuisha kuimarisha mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu, pamoja na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Iraq na waasi wa Syria.
Sheria hiyo, iliyopitishwa kwa kura 89 dhidi ya 11 katika baraza la seneti, inajumuisha ombi la rais wa Marekani Barack Obama la dola bilioni 5 kukabiliana na Dola la Kiislamu. Dola bilioni 3.4 kati ya kiwango hicho zitatengwa kwa ajili ya kuwapeleka wanajeshi wa Marekani kama sehemu ya harakati maalumu iliyopewa jina Operation Inherent Resolve, na dola bilioni 1.6 zitatumika kuwapa vifaa na kuvipa mafunzo vikosi vya Kikurdi kwa miaka miwili.
"Mashambulizi ya angani ya Marekani yaliubadili mkondo wa mapigano na kuyapa makundi yenye msimamo wa wastani fursa ya kujikusanya, lakini kundi la IS haliwezi kushindwa bila kikosi cha upinzani kulivamia," alisema Carl Levin, seneta wa chama cha Democratic, ambaye ni mwenyekiti wa kamati inayosimamia masuala ya majeshi ya Marekani.
"Ili kufanikisha hilo washirika wetu wa Kiarabu na Kiislamu lazima wawe msitari wa mbele kwasababu vita dhidi ya kundi la IS ni mapambano ndani ya Uislamu kwa ajili ya nyoyo na fikra za Waislamu."
Muswada huo unatoa bilioni 521.3 kwa matumizi ya jeshi na jumla ya dola bilioni 63.7 kwa harakati katika mataifa ya kigeni. "Muswada huu unajumuisha nyongeza ya mshahara kwa wanajeshi wa Marekani, unazipiga jeki juhudi zetu kuhakikisha wanajeshi wetu wako salama katika uwanja wa mapambano, na unaidhinisha fedha zinazohitajika kuimaliza kwa njia muafaka tume yetu nchini Afghanistan," alisema kiongozi wa maseneta walio wengi katika baraza la seneti, Harry Reid.
Gereza la Guantanamo halitafungwa
Licha ya upinzani kutoka kwa rais Obama, muswada huo unazuia mchakato wa kulifunga gereza la Guantanamo nchini Cuba. Muswada huo pia unazuia wafungwa wa Guantanamo kuhamishiwa Marekani. Haukutoa idhini mpya ya kutumia nguvu za kijeshi nchini Iraq na Syria kama alivyokuwa ameomba rais Obama, lakini spika wa bunge la Marekani John Boehner amemtaka Obama aliwasilishe suala hilo lijadiliwe katika bunge jipya mwaka ujao.
Marekani hutumia fedha nyingi zaidi kwa ajili ya jeshi lake kuliko taifa lolote ulimwenguni. Mnamo mwaka 2013, Marekani ilitumia dola bilioni 640 kwa ajili ya ulinzi, ikifuatiwa na China iliyotumia dola bilioni 188 na Urusi ikitumia dola 88, kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa shirika la kimataifa la utafiti wa amani mjini Stockholm nchini Sweden.
Mnamo mwaka 2013, Urusi iliwekeza asilimia kubwa zaidi ya pato jumla la taifa katika jeshi lake kufikia asilimia 4.1, ikiipiku Marekani ambayo ilitumia asilimia 3.8 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja.
Maoni
Chapisha Maoni