Azam FC yatimuliwa Uganda
SHIRIKISHO la Soka la Uganda (FUFA), limeizuia klabu
ya Azam FC kucheza mechi za kirafiki nchini humo kutokana na kutokuwa na
taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Azam ipo ziarani Uganda kwa ajili ya kambi ya wiki
mbili ikilenga kucheza mechi za kirafiki za kujipima nguvu dhidi ya timu
mbalimbali za nchi hiyo.
Tayari kikosi cha Wanalambalamba hao kimecheza
mchezo mmoja wa kirafiki kati ya minne iliyopanga kucheza dhidi ya SC Villa ambapo
ilidunguliwa mabao 3-2.
Pia ilipangwa kujipima dhidi ya timu za KCCA FC,
Viper na URA kabla ya kurejea nchini kuendelea na Ligi Kuu.
Msemaji wa FUFA, Ahmed Hussein alisema: “Hatujapata taarifa yoyote kutoka TFF kama kutakuwa na mechi zozote za Azam, hivyo tumeamua kuizuia hadi hapo watakapotutaarifu,” alisema Hussein.
Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alipoulizwa kuhusiana na taarifa hiyo ya FUFA alikana kuwa na taarifa za safari ya Azam kwenda Uganda.
“Utaratibu ni
kwamba timu yoyote inapokwenda kuweka kambi nchi nyingine ni lazima itoe
taarifa kwa chama cha soka mkoani kwake, Shirikisho la soka la nchi yake na
ndipo habari hizo zifike Shirikisho la Soka Afrika (CAF), alafu ziwafike
shirikisho la nchi wanayoenda ingawa ukanda huu wa Afrika Mashariki imekuwa
inachukuliwa kawaida.
“Kifupi hatujapata ujumbe huo kutoka FUFA, lakini
tutajitahidi kuwasiliana na Azam ili kujua namna ya kuwasaidia,” alisema
Mwesigwa.
Naye Ofisa Habari wa Azam FC, Jafari Idd ambaye
ameambatana na timu hiyo Uganda, alisema wao pia hawajapewa taarifa za kusitishwa
kwa mechi hizo na tayari wameshacheza
mchezo mmoja huku wakijiandaa kuikabili KCCA kesho Jumatano.-Hisani ya Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni