Wanawake waandamana kwenda msituni

ZAIDI ya wanawake 100 wa jamii ya Kimasai wameandamana kwenda kulala
msituni kwa siku mbili wakipinga kitendo cha serikali kukata miti ya asili katika Kijiji cha  Matebete, Kata ya Itamboleo, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.

Wanawake hao walichukua uamuzi huo jana, wakipinga hekta zaidi ya 32,000 za miti wanayoitegemea katika shughuli zao, kukatwa bila wao kushirikishwa.
 Mmoja wa wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina la Sofia Kalei, alisema hawako tayari kuona msitu huo ukiteketezwa kwa sababu umekuwa ukiwasaidia katika shughuli mbalimbali.

 “Serikali imeamua kukata miti katika msitu huu kwa kisingizio kwamba inataka kutengeneza madawati kwa ajili ya wanafunzi.
 “Tukiruhusu miti hii ikatwe, tutakuwa tukijimaliza wenyewe na tutakaoathirika zaidi ni sisi wanawake na siyo watu wengine.

“Kwa maana hiyo, ili kuonyesha jinsi tusivyokubaliana na uamuzi huu wa Serikali, tumeamua kuandamana na kuja msituni ili kupinga mpango huo wa Serikali,” alisema Kalei.
 Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matebete, Iman Tisho, alisema miti inayokatwa katika msitu huo itaendelea kukatwa kwa kuwa ni agizo la Serikali ya Wilaya ya Mbalali.

“Hili ni agizo la Serikali, lakini ikumbukwe kwamba, kabla ya kufikia uamuzi huu mimi na viongozi wenzagu tulikwenda wilayani kuwaeleza mpango huu nao wakatukubalia.

“Pamoja na kukubaliwa, tulipoleta wazo hilo hapa kijijini, wananchi waligoma na matokeo yake ndiyo hayo unayoyaona ambapo baadhi ya wananchi wameamua kuandamana kwenda msituni,” alisema Tisho.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4