Serikali yatakiwa kudhibiti ulevi Kilimanjaro
SERIKALI imetakiwa
kuingilia kati tatizo la ulevi wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, kwa kuwa
ulevi huo unachangia ongezeko la watoto yatima na wanaoishi katika mazingira
magumu.
Rai hiyoimetolewa leo
na Mwenyekiti wa asasi ya jinsia na maendeleo wilayani Rombo (AJIMARO) Athony
Massawe, wakati akikabidhi msaada wa chakula kwa watoto yatima na wale wenye
maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika Kituo cha Kulelea Watoto kiitwacho Cornel Ngaleku
cha wilayani hapa.
“Tatizo la ulevi kwa
wananchi wilayani hapa, linakua siku hadi siku na ni vema Serikali ikaingilia
kati na kulidhibiti, kwani limechangia maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na
kusababisha ongezeko la watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu.
“Tatizo hili pia limechangia
kiwango cha umasikini kuongezeka kwa wananchi, kwani vijana wengi ambao ndio
nguvu kazi ya taifa, wameathiriwa na pombe na wamesahau kufanya kazi kwa ajili
ya kujiletea maendeleo.
“Kutokana na tatizo
hilo, alisema asasi yake imejikita katika utoaji wa elimu kwa wananchi
juu ya athari za ulevi, ikiwa ni pamoja na namna ya kujikinga na maambukizi ya
ugonjwa wa Ukimwi ili kunusuru jamii hiyo,” amesema Masawe.
Katika hatua nyingine,
Massawe aliitaka jamii na taasisi mbalimbali nchini zione umuhimu wa
kuwasaidia yatima na wale waishio katika mazingira magumu, kwani wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa chakula.
“Tumetoa msaada wa
chakula kwa watoto hawa kwa kuwa tunatambua changamoto zinazowakabili. Kwa
hiyo, natoa wito kwa jamii na taasisi zote nchini zitenge muda wa kuwatembelea
na kutoa misaada mbalimbali kwa yatima, kwani nao wanahitaji kusaidiwa,”.
Awali akizungumza
wakati akikabidhiwa msaada wa chakula hicho, Sista Ritha Massawe alisema kituo
hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa chakula.
Maoni
Chapisha Maoni