Chama chamfukuza Rais
Guys Scott
CHAMA tawala cha nchini Zambia cha Patriotic Front (PF)
kimemfuta uanachama Rais wa mpito wa nchi hiyo, Guys Scott, kwa madai ya
kuvunja taratibu za kikatiba.
Kiongozi huyo aliyepewa jukumu la kuiongoza nchi hiyo baada
ya kifo cha Rais Michael Sata, anahusishwa na uvunjaji wa taratibu mbalimbali
za chama hicho, ikiwa ni pamoja na kufukuza ovyo wafanyakazi.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa PF, Malozo Sichone, ilieleza
Rais Scott amekuwa na tabia ya kuajiri na kufukuza viongozi katika muda mfupi
aliokaa katika uongozi wake.
“Scott amekuwa na tabia ya kuajiri na kuwafukuza watu kazi ovyo
bila ya kushauriana na Kamati Kuu ya chama,” alisema Sichone.
Alisema licha ya kutimuliwa ndani ya chama, lakini ataendelea
kuwa mwanachama wa chama hicho katika kipindi cha mpito cha urais wake hadi Januari
20, 2015, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Rais Scott hataweza kuwania kiti hicho kupitia PF kutokana
na kukosa sifa inayomtaka kuwa na wazazi wazawa wa nchi hiyo.
Kutokana na tabia ya Scott, kumetokea makundi ya
waandamanaji katika barabara za Lusaka.
Scott amekosa uungwaji mkono na wanachama wa chama hicho,
huku wakimuunga mkono Edgar Lungu, aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo wakati Sata
alipokuwa hospitali mjini London.
Scott, ambaye wazazi wake ni Waingereza, ameweka historia
kwa kuwa Mzungu wa kwanza kushikilia nafasi hiyo baada ya nchi zote za Afrika
kupata uhuru.
Maoni
Chapisha Maoni