Bahrain kuwachukulia hatua waliosusia uchaguzi
Waziri wa Sheria wa Bahrain ametaka watu wote waliokataa
kushiriki kwenye uchaguzi wa Bunge uliofanyika hivi karibuni nchini humo
kuchukuliwa hatua kali za kisheria.Khalid bin Ali Aal Khalif
Khalid bin Ali Aal Khalifa ameyasema hayo mbele ya kikao cha baraza
la mawaziri kilichofanyika mjini Manama. Pendekezo hilo la Waziri wa
Sheria wa Bahrain la kuchukuliwa hatua wale wote waliokataa na kususia
uchaguzi wa Bunge, tayari limewasilishwa mbele ya kamati ya sheria ya
baraza la mawaziri. Imeelezwa kuwa, duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge
wa kimaonyesho iliyofanyika siku ya Jumamosi iliyopita nchini Bahrain,
iliwashirikisha watu laki tatu na elfu hamsini. Duru ya pili ya uchaguzi
huo, imepangwa kufanyika Jumamosi ijayo. Serikali ya Bahrain ilitangaza
kwamba asilimia 51.5. ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura
walishiriki kwenye uchaguzi huo, ilhali, chama kikuu cha upinzani cha al
Wifaq nchini Bahrain kilitangaza kuwa, karibu asilimia 30 tu ya watu
ndiyo iliyoshiriki kwenye uchaguzi huo wa kimaonesho na wengi wao wakiwa
ni wanajeshi na wafanyakazi wa serikali. Inafaa kuashiria hapa kuwa,
tokea mwezi Februari mwaka 2011, nchi hiyo ya Kiarabu imegubikwa na
maandamano ya wananchi wanaotaka mfumo wa kidemokrasia sanjari na
kuondoshwa madarakani utawala wa kifalme wa Aal Khalifa.
Maoni
Chapisha Maoni