Mathias Chikawe akemea ndoa za utotoni
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Tanzania amepinga vikali tabia ya baadhi ya wazazi ya kuwaozesha watoto wao wakiwa na umri mdogo. Mathias Chikawe amesema hayo alipokuwa akizungumza na wakimbizi wa kambi ya Nyarugusu huko Kigoma na kuwataka wakimbizi hao kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wenye umri mdogo kwa kuwa ni kuwaingiza katika matatizo wakati wa kujifungua. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Tanzania amewataka wazazi nchini humo wawape haki watoto wao na kwamba, utamaduni wa kuwaozesha watoto wadogo sio mzuri kwani huwafanya watoto hao kukumbwa na matatizo mengi hasa wakati wa kujifungua. Wakati huo huo imeelezwa kwamba, umasikini na ukosefu wa elimu juu ya ukatili wa kijinsia miongoni mwa wanajamii nchini Tanzania ni miongoni mwa sababu zinazochangia watoto wadogo kukumbana na ndoa za utotoni. Aidha mila potofu na utamaduni mbovu wa baadhi ya makabila nchini humo inaelezwa kuwa sababu nyingine inayochangia tatizo hilo.
Maoni
Chapisha Maoni