Ni gari la polisi au Rais lililoibiwa Kenya?
Taarifa hii ilitolewa na baadhi ya vyombo vya habari ingawa msemaji wa Rais Kenyatta ameikanusha taarifa hiyo akisema kuwa gari lililoibiwa lilikuwa la idara ya polisi likiendeshwa na inspekta mkuu wa polisi.
Gari hilo lililokuwa lisemekana kuwa na uwezo wa kuhimili risasi, liliibiwa usiku wa Jumatano na kwamba aliyekuwa analiendesha gari hilo alikuwa afisa wa polisi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Daily Nation ikimnukuu mtu anayesemekana kuwa dereva wa gari hilo la kifahari alilazimishwa kuvua nguo zake kabla ya kupokonywa gari hillo.
Gari lenyewe lilikuwa na nambari ya usajili ya kibinafsi.
Ni gari la polisi au la Rais?
Kwa mujibu wa msemaji wa Rais, gari hilo aina ya BMW 735 la mwaka 2000, lilikuwa linaendeshwa na inspekta wa polisi alipovamiwa na wanaume wanne waliokuwa wamejihami karibu na eneo la Ruai viungani mwa mji mkuu Nairobi.
Msemaji wa Rais Manoah Esipisu amekanusha madai kwamba gari hilo lilikuwa moja ya magari ya ulinzi wa Rais Uhuru Kenyatta kama ilivyokuwa imenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari
Bwana Manoah amesema kuwa Inspekta aliyekuwa anaendesha gari hilo aliporwa dola miasaba na simu yake gari hilo lilipoibiwa saa tatu usiku. Alitekwa na majambazi hao kwa karibu saa tano kabla ya kumwachilia usiku wa manane. Alisema kuwa wezi hao walitoweka na gari hilo ambalo alisema hutumiwa kwa shughuli za polisi na kwamba tayari msako umeanzishwa ingawa gari hilo bado halijapatikana.
Kadhalika alikanusha kuwa gari hilo lilikuwa la ulinzi wa Rais na kwamba lenyewe lilikuwa na uwezo wa kuhimili risasi.
Visa vya wizi wa magari na utekaji wa madereva sio jambo geni nchini Kenya ila kilichowashangaza wengi ni kwamba je viopi gari la ulinzi wa Rais liibiwe?
Bwana Manoah amesema takwimu zinaonyesha visa vya uhalifu vimepungua hasa katika jiji kuu Nairobi katika miezi ya hivi karibuni na kwamba ulinzi unaendelea kuimarishwa.-bbc
Maoni
Chapisha Maoni