Wazazi wakijia juu Chuo Kikuu St. John

Wazazi wa wanafunzi waliomaliza ngazi ya Stashahada mwaka 2012/2014 katika Chuo Kikuu cha St. John (St Mark’s), Kampasi ya Buguruni Malapa, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam wamekuja juu wakisema kama matokeo ya watoto wao hayatapelekwa katika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) ili kuomba kujiunga na vyuo vikuu kwa wakati ifikapo kesho, watachukua hatua za kisheria dhidi ya chuo hicho.

Walitangaza azma hiyo jana kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu walizopiga katika chumba cha habari cha NIPASHE kufuatia habari iliyochapishwa na gazeti hili jana kuhusu hofu ya wanafunzi hao kukosa kujiunga vyuo vikuu kutokana na chuo hicho kuchelewa kupeleka matokeo ya wanafunzi Nacte kama sheria inavyotaka.

“Ikifika tarehe 31 Julai (kesho) kama watakuwa hawajapeleka matokeo Nacte kwa wakati lazima sheria ichukuwe mkondo wake ili kuwasaidia wanafunzi kupata haki yao,” alisema mmoja wa wazazi hao.

Kabla ya wazazi hao kuja juu, baadhi ya wanafunzi walitoa malalamiko kupitia gazeti hili wakihofia kukosa kujiunga na vyuo vikuu kutokana na chuo hicho kuchelewa kupeleka matokeo yao Nacte, huku kesho ikiwa ni siku ya mwisho kuwasilisha maombi ya kujiunga na vyuo vikuu yakiwa yameambatanishwa na matokeo yenye muhuri wa chuo.

Wanafunzi hao walisema uongozi umekuwa ukiwazungusha kuwapa matokeo wakati wameshayalipia benki Sh. 10,000 na kupeleka nakala ya stakabadhi za malipo hayo chuoni.

Naibu Mkurugenzi wa Chuo hicho, Kampasi ya Dar es Salaam, Mwalimu Amani Chipato, akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Naom Katunzi, juzi alisema matokeo yameshatolewa, lakini hayajapelekwa Nacte.

Alisema hiyo inatokana na chuo kuchelewa kupata taarifa mapema za mabadiliko ya kukabidhi matokeo Nacte ili yawekwe kwenye mfumo wa mtandao.

Akijibu swali jinsi gani watawasaidia wanafunzi kupeleka maombi vyuoni kabla ya kesho, Mwalimu Chipato alisema: “Ikitokea imeshindikana hakuna namna”.

Hata hivyo, alisema Nacte hawapaswi kulaumiwa, kwani mfumo wa chuo ndiyo unaokabiliwa na tatizo la mawasiliano kati ya makao makuu, mkoani Dodoma na Kampasi ya chuo cha Dar es Salaam.
 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4