Madaktari wasubiri uchunguzi IMTU
Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU)
cha Dar es Salaam wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jana.
Dar es Salaam. Baraza la Madaktari Tanganyika
(TMC) limesema linasubiri majibu ya ripoti zilizoundwa kuchunguza sakata
la utupaji holela wa viungo vya binadamu, kabla ya kutoa adhabu
stahiki kwa madaktari waliohusika.
Msajili wa baraza hilo, Peter Luena alisema
ingawa ofisi yake haina mamlaka ya kukichukulia hatua za kinidhamu Chuo
Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) kinachodaiwa kutupa
viungo hivyo, inao uwezo wa kutoa adhabu za aina nne kwa madaktari
watakaobainika kuhusika.
Wiki iliyopita Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
na Jeshi la Polisi waliunda timu mbili tofauti kuchunguza namna ambavyo
viungo vya binadamu kutoka IMTU vilivyotupwa katika Bonde la Mto Mpiji,
jijini Dar es Salaam.
Luena alisema maadili ya udaktari yanaeleza kuwa
iwapo daktari amekiuka taratibu za kazi ataitwa mbele ya Baraza la
Madaktari na kusomewa mashtaka yake.
“Iwapo atapatikana na kosa, sheria yetu ina hatua
nne za adhabu; onyo la kawaida, karipio kali, kusimamisha usajili wa
daktari husika na kama ni kosa kubwa anafutiwa usajili kabisa,” alisema.
Hata hivyo, alisema daktari atakayepewa adhabu
anaweza kujitetea na kuomba apunguziwe adhabu husika, akikataliwa
anaweza kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania.-Mwanchi
Maoni
Chapisha Maoni