Yanga yapata ulaini Tunisia
YANGA imepata mteremko kuelekea mchezo wao wa
marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile ya Tunisia, kwani
imepata mbinu zitakazowawezesha kuwashika pabaya wapinzani wao hao.

Mchezo huo ni wa raundi ya pili ya michuano hiyo
ambapo katika mchezo wa kwanza uliopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Matokeo hayo yanaipa kibarua kigumu Yanga mjini
Tunis kwani watalazimika kushinda au kupata sare ya zaidi ya mabao 2-2 ili
iweze kusonga mbele na kutinga hatua ya mtoano kuwania tiketi ya makundi.
Kwa kufahamu ugumu wa mchezo wa marudiano, Yanga
imepanga kufanya kila mbinu wanazoweza ili kuwajengea mazingira mazuri ya
kushinda na kuwatoa Etoile.
Miongoni mwa mbinu hizo ni kuwahi mapema nchini
Tunisia ili kuzoea hali ya hewa ya huko ambayo ni ya baridi na kukutana na Watanzania
waishio huko ili waweze kuwapa mikakati ambayo wanaweza kuitumia kukwepa hila
za wapinzani wao hao na kushinda.
Lakini pia, Yanga imepanga kujenga urafiki na
wapinzani wakubwa wa Etoile, Esperance Sportive de Tunis (ES Tunis) ili kuona
ni vipi wanaweza kushirikiana nao wawape mbinu za kufanya vema katika mchezo
wao huo ujao.
Akizungumza na BINGWA, Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas
Tiboroha, alisema: “Bado tuna matumaini ya kuwatoa Etoile, tumepanga mikakati
ya kutosha kutuwezesha kushinda ugenini, ikiwamo kuwahi kwenda Tunisia ili
kuzoea hali ya hewa ya kule, kuwatumia Watanzania waliopo mjini Tunis kufahamu
ni vipi tunaweza kuwashinda wapinzani wetu.
“Lakini pia tukiwa huko tutakutana na wapinzani
wakubwa wa Etoile kuona ni vipi tunaweza kushirikiana nao watusaidie kutupa
mbinu za kuwatoa wapinzani wetu.”
Tiboroha alisema kwa jinsi walivyojipanga, hawadhani
kama wanaweza kutolewa kirahisi na Etoile kwani hata Kocha Mkuu wao, Hans van
der Pluijm amewahakikishia kutekeleza majukumu yake kuelekea mchezo huo.
ES Tunis ni miongoni mwa timu kongwe Tunisia ikiwa
inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ya nchi hiyo kutokana na
kujizolea pointi 49 ndani ya mechi 24, sawa na Club Africain iliyopo nafasi ya
pili kwa wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Etoile wao ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi
50 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Na leo Etoile du Sahel watavaana na ES Tunis katika pambano
la kukata na shoka ambapo kila timu itapania kushinda ili ijiweke katika
mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
Iwapo ES Tunis itashinda, itakuwa imefanikiwa
kuongoza ligi hiyo kwa kufikisha pointi 51, lakini kama Etoile wataibuka
kidedea, watakuwa wamezidi kujikita kileleni mwa ligi hiyo kwa kuwa na pointi
54.
Maoni
Chapisha Maoni