Simba yaipumlia Azam
KLABU ya soka ya Simba imeendeleza kampeni zake za
kuwania nafasi ya pili katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana
kuishindilia Mgambo JKT mabao 4-0, huku mshambuliaji wake hatari, Emmanuel Okwi,
akiondoka na mpira kwa kupachika wavuni mabao matatu.
Mchezo huo wa marudiano umepigwa kwanye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam leo, ambapo
Simba walikuwa wamepania kulipiza kisasi cha kufungwa mabao 2-0 katika
mchezo wa awali uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Matokeo ya ushindi wa leo yameiwezesha Simba kufikisha
pointi 38 na kuongeza ushindani wa kuchuana vikali na mabingwa watetezi wa ligi
hiyo, Azam FC, kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Simba na Azam wametofautiana kwa pointi nne tu,
ambapo Azam wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 42 baada ya kushuka
dimbani mara 22, huku wapinzani wao wakiwazidi kwa mchezo mmoja.
Okwi aliandika bao la kuongoza kwa Simba dakika ya
nane, akiunganisha pasi safi ya Hassan Ramadhani Kessy na kuachia shuti
lililotinga moja kwa moja wavuni.
Simba nusura wapachike wavuni bao la pili dakika
ya 10 kupitia kwa Okwi tena, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango huku kipa
wa Mgambo JKT, Godson Mmasa akiwa tayari ametoka golini kwake.
Kiungo mshambuliaji Ramadhani Singano ‘Messi’, ambaye
alipiga mpira wa adhabu ndogo aliwaamsha mashabiki wa Simba dakika ya 25, baada ya kupiga shuti lililogonga
mwamba na kutinga wavuni na kumuacha kipa wa Mgambo akishangaa asijue cha
kufanya.
Dakika ya 40 Okwi alifunga bao la tatu, baada ya
kuwatoka mabeki wa Mgambo ambao walishindwa kumkaba na kuwapiga chenga, kabla
ya kuachia shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.
Salum Gila wa Mgambo alijaribu bahati yake kutaka
kuiandikia bao timu yake dakika ya 43, lakini shuti lake lilipaa juu na kutoka
nje, hivyo kuifanya Simba kwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao 3-0.
Katika mchezo mwingine wa ligi uliochezwa
kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wenyeji Polisi Morogoro walitoka suluhu na
Coastal Union na kuzidi kujiweka katika mazingira mabaya ya kushuka daraja
msimu huu.
Maoni
Chapisha Maoni