Mabeki Yanga wamchefua Pluijm
KOCHA Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans van Der Pluijm,
ameelezea kukerwa na uzembe uliofanywa na mabeki wake wa kuruhusu kufungwa
kirahisi, huku akionyesha hali ya ukali kwa kila mchezaji aliyeshindwa kutimiza
majukumu yake ipasavyo.

Pamoja na makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa
juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga
waliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Stand United.
Akizungumza jijini Dar es Salaam , Pluijm
alikiri kuwa kikosi chake kilikuwa na bahati ya ushindi katika mchezo huo licha
ya upinzani mkali walioupata kutoka kwa wachezaji wa Stand ambao walicheza kwa
kiwango cha juu.
Alisema kiungo Simon Msuva na mshambuliaji Amissi
Tambwe walikosa nafasi za wazi, ambazo zingeweza kuongeza idadi ya mabao huku
akidai soka ni mchezo wa makosa siku zote hivyo lolote linaweza kutokea.
Pluijm aliendelea kusisitiza kwamba, mawasiliano ni
kitu muhimu kwa wachezaji wanapokuwa uwanjani, huku akiwashushia lawama wale
walioonekana kufanya uzembe wa wazi na kupelekea kufungwa mabao hayo.
Wakati Pluijm anafanya mabadiliko ya kumtoa kiungo
Mbrazil, Andrey Coutinho ambaye alionekana bado hajarejea katika kasi yake na
kumuingiza Mliberia, Kpah Sherman, hakusita kumweleza makosa ya wazi aliyokuwa
akifanya.
Pia Mholanzi huyo hakufurahishwa na baadhi ya
matukio yaliyofanywa na beki Mbuyu Twite, ambaye alimpa maneno ya ukali baada
ya pambano hilo kumalizika wakati wachezaji wakielekea kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo.
Alisema atahakikisha anakutana na wachezaji wake na
kuzungumza juu ya umuhimu wa kuwepo na mawasiliano uwanjani, ili kuondoa tatizo
sugu linalowasumbua kwa muda mrefu sasa.
Yanga ambao wanahitaji pointi sita kuwa mabingwa
msimu huu, wanatarajiwa kushuka dimbani tena kesho kuwakabili maafande wa Ruvu
Shooting kabla ya kuwavaa Polisi Morogoro wiki ijayo.
Kwa ushindi huo, Yanga wameendelea kutesa kileleni
mwa Ligi Kuu, wakiwa na pointi 49 ikiwa ni tofauti ya pointi saba dhidi ya Azam
FC wanaoshika nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 42.
Maoni
Chapisha Maoni