Anna Kilango ajipigia debe
MBUNGE wa Same Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Anna Kilango Malechela, amesema anawacheka watu wanaopita
jimboni kwake na kutangaza kuwania ubunge katika jimbo hilo.

Kilango alitumia fursa ya ziara yake ya mara ya kwanza katika
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kujipigia debe ambapo alisema kujituma kwake na
kufanya kazi aliyotumwa na wananchi vizuri ndiko kunakompa kujiamini kuwa
atachaguliwa tena.
Kilango alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na
wafanyakazi wa Mamlaka hiyo hivi karbuni ambapo aliwaasa kufanya kazi kwa
kujituma kwani ndio msingi wa mafanikio ukiachilia mbali changamoto zilizopo.
“Mtu anayefanya kazi vizuri anakuwa na amani na hana wasiwasi.
Hata mimi najua kuna watu wanajipitisha huko jimboni wanataka ubunge lakini
mimi nawacheka tu kwa sababu sina wasiwasi na wala siwezi kujibizana nao.
Ikifika hiyo siku ya kujinadi nitawaeleza wananchi nilichofanya na naamini
watanichagua tena kwa sababu nimefanya kazi nzuri,” alisema Kilango.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Naomi Katunzi
alisema Mamlaka hiyo inachangamoto ya uhaba wa rasilimali fedha kwakuwa
mahitaji ya taasisi za elimu ni mengi na hivyo kuwataka wadau na wananchi
kuchangia elimu kupitia mfuko wa elimu uliopo chini ya mamlaka hiyo.
“Tunaomba watanzania wawe na moyo wakuchangia elimu kama
wanavyochangia kwenye harusi na sherehe zingine,” alisema Katunzi na kuongeza,
“kwa sasa tunapokea fedha kidogo sana kutoka kwa wadau wakiwemo wananchi lakini
bado tunawahamasisha waendelee kujitoa kama wenzetu wa mataifa ya magharibi
wanavyofanya na ndio maana wameendelea sana kielimu.”
Maoni
Chapisha Maoni