Yanga yawashika pabaya simba kwa okwi
MSHAMBULIAJI hatari wa Simba, Emmanuel Okwi,
amefichwa katika moja ya hoteli za kifahari jijini Dar es Salaam, huku Yanga
wakitajwa kuhusika na hatua hiyo.
Tukio hilo limekuja zikiwa ni siku chache kabla
ya Simba kuvaana na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili hii.
Sababu za Yanga kuhusika na kufichwa kwa Okwi, zinatokana
na undugu baina yao, kwani alishawahi kufanya kazi Jangwani, lakini pia
akitajwa kuwa na uhusiano mzuri na baadhi ya wanachama na matajiri wa klabu
hiyo.
Ni kutokana na kufahamu hilo, uongozi wa Simba
juzi ulifanya uamuzi wa ghafla kwa kuwapeleka katika hoteli maalumu Okwi na
wachezaji wenzake wa Uganda, Danny Sserunkuma na Jjuuko Murushid, ili kuvuruga
mawasiliano yoyote yanayoweza kufanywa baina ya Yanga na Okwi.
Uongozi wa Simba unafahamu kuwa iwapo Yanga
watapata fursa ya kukutana na Okwi, wanaweza kumrubuni ili kucheza chini ya
kiwango au kuwasaidia kwa njia yoyote ile kuepuka kipigo siku hiyo.
Mmoja wa kiongozi kutoka ndani
ya klabu hiyo, alilipasha BINGWA kuwa uamuzi wa kuwaficha wachezaji hao umekuja
mara baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Tanzania Prisons.
“Tunajua fitna za wapinzani wetu,
Yanga, ndio sababu ya kuamua uamuzi huu wa kuwaweka wachezaji hao kwenye hoteli
ya pamoja ili kuepuka hujuma,” alisema.
Chanzo hicho kilisema kikosi cha timu hiyo
kimeondoka asubuhi kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kambi ya kusubiri mechi hiyo
inayosubiriwa na mashabiki mbalimbali.
BINGWA lilimtafuta Katibu wa Simba, Stephano Ali
kuzungumzia kambi hiyo ya Zanzibar na kusema kikosi hicho kimeondoka na
wachezaji wote, kasoro Simon Sserunkuma aliyekuwa nchini Uganda kwa matatizo ya
kifamilia.
Alisema kikosi hicho kimeondoka na Kocha Msaidizi,
Suleimani Matola, huku kocha mkuu, Kopunovic akiomba kupumzika kwa siku mbili
jijini Dar es Salaam kabla ya kuungana na wachezaji wake.
“Timu imeondoka saa 6:00 wakati mkutano mkuu
ukiendelea na imeondoka na Matola, huku Kocha Mkuu akitarajiwa kuungana na timu
yake keshokutwa,” alisema.
Simba inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi
hiyo ikiwa na pointi 24, baada ya kushuka dimbani mara 16, wakati Yanga wakiwa
kileleni na pointi zao 31 kutokana na mechi 15.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni