Okwi: akili kubebwa J’mosi
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba, Emmanuel Okwi,
amemshukuru mwamuzi wa mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar uliochezwa Jumamosi
iliyopita, Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, kwa kuongeza dakika tano baada ya
dakika 90 za muda wa kawaida, hivyo kuwawezesha kufunga bao pekee lililoipa timu
yake ushindi wa 1-0.

Okwi alifunga bao hilo dakika ya tatu kati ya
tano za muda wa nyongeza, wakati timu hizo zikiwa hazijafungana katika mchezo
huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mganda huyo alifunga bao hilo kwa staili ya aina
yake, akipiga shuti kali akiwa umbali wa mita 25 kutoka lango la Mtibwa baada
ya kupokea pasi kutoka kwa Abdi Banda.
Kabla ya kufunga bao hilo wakati baadhi ya
mashabiki wakiwa wametoka uwanjani wakijua matokeo ni suluhu, aliwahadaa mabeki
na kumchungulia kipa wa wapinzani wao hao alivyokaa na kupiga mpira mrefu
uliokwenda moja kwa moja wavuni.
Okwi alisema miongoni mwa watu anaowashukuru kwa kumpa nguvu ya kutafuta bao ni
mwamuzi huyo, baada ya kuongeza dakika hizo tano.
Alisema anaamini kama mwamuzi asingeongeza muda
huo, wangeweza kutoka suluhu na Mtibwa kwa kuwa mchezo ulionekana kuwa mgumu
kwa pande zote tangu dakika ya mwanzo.
“Nilishakata tamaa ya kufunga hadi pale mwamuzi
wa pembeni alipoonyesha dakika tano za nyongeza ndipo nilipoona naweza kufanya
kitu kuleta furaha Msimbazi, nashukuru hilo limewezekana, hii ni ishara tosha
kuwa tunaweza kumaliza ligi katika nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa
mwakani,” alisema.
Ushindi wa Simba juzi, umeiweza timu hiyo kupanda
hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi
29 ndani ya michezo 18, nyuma ya Azam wenye pointi 30, kabla ya mchezo wao wa
jana na Yanga waliokuwa kileleni wakiwa na pointi 31.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni