Ngassa alamba dume TP Mazembe
MABAO sita aliyofunga msimu uliopita katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na matatu ya Kombe la Shirikisho msimu huu,
yamemsafishia njia Mrisho Ngassa kutua TP Mazembe ya DRC, ikiwa ni kutokana na
mpango unaosukwa na Mtanzania Mbwana Samatta, anayeichezea timu hiyo.
Msimu uliopita, Ngassa aliifungia Yanga mabao
hayo ndani ya mechi nne za hatua ya awali na ya kwanza na kumfanya kuwa
miongoni mwa wafungaji bora wa michuano hiyo.
Kutokana na mafanikio hayo, mawakala wa klabu
mbalimbali barani Afrika na kwingineko, walianza kufuatilia nyendo za straika
huyo kuona kama ana kiwango cha kumwezesha kuzichezea timu zao.

Na kwa kuwa Samatta naye anatoka Tanzania,
waliamua kumtumia kujua ubora wa winga huyo machachari.
Kutokana na hilo, Samatta alimtumia ujumbe Ngassa
kumtaka kudhihirisha ubora wake wa kucheka na nyavu msimu huu wakiwa wanashiriki
michuano ya Kombe la Shirikisho, jambo ambalo mkali huyo amelifanya ndani ya
mechi tatu za kwanza kwa kufunga mabao matatu.
Ngassa alifunga bao lake la kwanza katika mchezo
wa marudiano wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya BDF XI nchini Botswana,
kabla ya juzi kucheka na nyavu mara mbili walipoivaa FC Platinum ya Zimbabwe
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa raundi ya kwanza ya michuano
hiyo, Yanga walishinda mabao 5-1 na hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya
kutinga raundi ya pili kuelekea mchezo wa marudiano unaotarajiwa kupigwa kati
ya Aprili 1 na 3, mwaka huu.
Akizungumza na BINGWA kabla ya mchezo wa Yanga wa
juzi, Samatta alisema: “Mawakala wa timu mbalimbali watakuwa wakimfuatilia
Ngassa kwa karibuni mno, hivyo ni jukumu lake kuhakikisha anazidi kufunga ili
kujisafishia njia kwa kufunga mabao mengi katika hatua hizi za awali.”
Na kama alivyokuwa akishauri mkali huyo wa TP
Mazembe, Ngassa alifanya kweli kwa kufunga mabao hayo, lakini pia akicheza kwa
kiwango cha juu kwa kutengeneza mengine mawili yaliyofungwa na Niyonzima na
Tambwe.
Japo Samatta hakuweka wazi, lakini inaonyesha
Mtanzania huyo ameanza kumpigia debe Ngassa katika kikosi chao, akiamini
wanaweza kutengeneza kombinesheni kali kama wawapo pamoja katika kikosi cha
timu ya Taifa, Taifa Stars.
Tayari Ngassa ameonyesha dalili za kutoendelea
kuichezea Yanga baada ya kumalizika kwa mkataba wake mwishoni mwa msimu huu na
kuna taarifa kuwa klabu kadhaa zimeanza kumwinda, ikiwamo Free State ya Afrika
Kusini.
Kwa siku za hivi karibuni, Ngassa amekuwa moto wa
kuotea mbali, akichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa timu yake hiyo kwenye
Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.-Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni