Kocha Platinum ajuta kuifahamu Yanga
KOCHA wa Platinum ya
Zimbabwe, Norman Mapeza, amesema hatakisahau kikosi cha Yanga kutokana na
kuwafanyia mauaji katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Kombe la
Shirikisho barani Afrika, uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Norman Mapeza |
Katika mchezo huo
uliokuwa na msisimko wa aina yake, Yanga ilishinda mabao 5-1, wafungaji wakiwa
ni Salum Telela, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe na Mrisho Ngassa, aliyecheka na
nyavu mara mbili.
“Nimekuja Tanzania nikitambua nakuja kucheza na timu imara, nikawasisitiza
wachezaji wangu kuwa makini kuepuka kufungwa mabao mengi, lakini wameshindwa na
kujikuta tukifungwa mabao mengi.”
Alisema kuwa kikosi
kizima cha Yanga kinatisha, hivyo hawezi kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja,
zaidi ya kuona wanakwenda kujipanga vipi kwao waweze kulipiza kisasi.
Aliionya Yanga kutobweteka
na ushindi wao huo na kujiona wamefanikiwa kuwatoa, kwani iwapo wao wameweza
kupata mabao matano wakiwa nyumbani kwao, nao hawashindwi kupata idadi kama
hiyo wakiwa Zimbabwe.
Wakati huo huo, Haruna
Niyonzima amesema siri kubwa ya ushindi mnono walioupata juzi ni mshikamano na
umoja walioonyesha wachezaji na viongozi wao.
“Umoja na mshikamano
ambao wachezaji na viongozi wameuonyesha ndio umetupa mafanikio haya ya kupata
ushindi mkubwa, kikubwa tuendelee kushikamana Wanayanga kazi bado ni ngumu
mbeleni,” alisema Niyonzima.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni