Watuhumiwa sita wa ugaidi wapandishwa kizimbani
WATU sita wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya
ugaidi kwa kutegesha na kulipua mabomu yaliyotengenezwa kienyeji katika matukio
matatu tofauti mkoani Ruvuma, jana wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
wa Mkoa wa Ruvuma kujibu mashtaka yanayowakabili huku nje kukiwa na ulinzi
mkali wa Jeshi la Polisi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Simoni Kobelo,
Mwendesha Mashtaka ambaye pia ni
Wakili Mfawidhi wa Serikali wa Kanda ya
Ruvuma, Silivanus Mkude, aliwataja watuhumiwa hao
kuwa ni Juma Kibwana maarufu kwa jina la Msabila, Mwalimu Yusuph na Hamza
Singano ambao ni wakazi wa Majengo, Manispaa ya Songea, Yasin Musa maarufu kwa
jina la Kafupi ambaye ni mkazi wa Manispaa ya Songea, Hasan Mponda na Said
Mhando.
Wakili Mkude alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa
wote wanakabiliwa
na mashtaka matatu tofauti ya kujaribu kuwaua askari
polisi waliokuwa doria na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani waliokuwepo
kazini katika eneo la Mshangano Manispaa ya Songea.
Alidai kuwa kosa la kwanza la kujaribu kuua
lilitokea Desemba 25, mwaka jana katika eneo la Mtaa wa Kotazi Majengo na mmoja
kati yao alijaribu kuwarushia askari polisi bomu lililotengenezwa kienyeji
waliokuwa wanafanya doria na kabla hajafanikiwa lilimlipukia na kumsababishia
kifo na askari polisi wawili walijeruhiwa.
Alitaja shtaka la pili kuwa Oktoba 27, mwaka jana
saa 10 jioni walichimbia ardhini bomu la kienyeji katika eneo la Mshangano
kando kando ya barabara ya kutoka Songea kwenda Njombe ambalo hutumiwa na
askari wa Usalama Barabarani kama kituo cha ukaguzi wa magari yanayotoka na
kuingia Songea Mjini kwa lengo la kuwalipua askari na kabla hawajatimiza lengo
lao askari waligundua na kulitegua bomu hilo.
Alilitaja shtaka la tatu linalowakabili kuwa
inadaiwa Septemba 16, mwaka jana saa 12 jioni katika Kata ya Misufini karibu na
Matarawe Songea Mjini, waliwarushia bomu la kienyeji askari waliokuwa kazini na
kuwajeruhi.
Kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza
kesi za ugaidi, washtakiwa hawakuweza kujibu mashtaka yanayowakabili na kesi
hiyo itatajwa tena Februari 19, mwaka huu na washtakiwa wote wamepelekwa
mahabusu baada ya kukosa dhamana.-Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni