Wananchi wamuua aliyemuua polisi
MTUHUMIWA Tissi Mallya ambaye alitoroka baada ya kumuua
polisi, G.7168 Koplo Joseph Swai,
ameauwa usiku wa kuamkia jana na wananchi alipokuwa amejificha akiwa na panga
lenye damu lililotumika kwenye mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime alisema hayo jana
katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP), Ernest Mangu, akiaga mwili wa Askari Joseph Swai, aliyeuawa wakati akijaribu kumwokoa mtoto aliyetaka kuchinjwa na baba yake mkoani Dodoma jana |
Mauaji hayo yalitokea juzi asubuhi
katika eneo la Chang’ombe Juu.
Kamanda Misime alisema baada ya
Malya kutekeleza mauaji hayo alikimbia lakini ilipofika saa 5.00
usiku wananchi walimuona maeneo ya Mtimkavu Mailimbili akiwa bado na panga
alilotumia kumuua Koplo Joseph.
“Wananchi walichukua sheria mkononi
na kumshambulia hadi polisi walipofika eneo la tukio wakamchukua na kumkimbiza katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma lakini aligundulika tayari amekwisha kufariki
dunia,” alisema.
Kamanda Misime alisema katika kumbukumbu zilizopo, mwaka 2006 Mallya aliwahi kufungwa miaka
mitatu kwa kujeruhi, pia mwaka 2009
alifungwa miezi sita kwa kutishia kuua.
“Nawapongeza wananchi walioonyesha
kuchukizwa na kitendo alichotendewa
askari wetu lakini waache kujichukulia sheria mkononi,” alisema.
Pia alitoa wito kwa wananchi kuchukua hatua kurekebisha maadili kuanzia
ngazi ya familia kwa sababu imebainika mtuhumiwa alikuwa mvuta bangi kiasi kwamba alikuwa anafanya vitendo ambavyo ni
kinyume na maadili ya jamii.
Diwani
wa Kata ya Mnadani, Steven Masangia, alisema alimfahamu polisi aliyeuawa kama
kijana mchapakazi ambaye alijitolea kutoa elimu hata kwenye mitaa juu ya ulinzi
shirikishi.
“Alipokuwaa Mnadani alipambana kuhakikisha
uhalifu unakomeshwa na hata vijana wanaovuta bangi aliwasambaratisha, na
alikuwa akifundisha polisi jamii kwenye mitaa ya kata,” alisema na kuongeza:
“Alikuwa na cheo kidogo lakini kazi alizokuwa
akifanya zilikuwa ni kubwa ikilinganishwa na cheo na umri wake” alisema .
Katika mkasa huo uliotokea juzi
asubuhi, askari huyo aliitikia wito wa
kuwapo kwa dalili za tendo la jinai nyumbani kwa mkazi mmoja wa Chang’ombe Juu.
Alipofika nyumbani kwa mkazi huyo
ndipo mkasa huo ulipomtokea alipotaka kumuokoa mtoto mchanga ambaye alikuwa
auawe na baba yake kwa panga.-mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni