Twiga Cement chafungwa muda usiojulikana
Kiwanda cha saruji cha Twiga Cement cha jijini Dar
es Salaam, kimepigwa marufuku kuzalisha sementi kutokana na kusambaza
vumbi la linalohatarisha afya za watu na kuchafua mazingira.
Amri ya kukifungia kiwanda hicho kwa muda usiojulikana ilitolewa
jana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na
kukiagiza kulipa faini ya Shilingi milioni 50 kwa kuvunja sheria.

‘Twiga Cement’ kwa mujibu wa NEMC inachafua mazingira na imeshindwa
kudhibiti vumbi linalotokana na uzalishaji wa sementi linalopitia
kwenye bomba lililoelekezwa angani.
Kiwanda hicho cha Twiga Cement ambacho kipo eneo la Wazo Hill nje
kidogo ya Dar es Salaam kinahusishwa na kutodhibiti vumbi linalosaabisha
watu kupata maradhi.
Kiwanda hicho kiliamriwa kulipa mara moja faini ya Shilingi
milioni 50 kwa kuvunja kifungu namba 191 cha sheria ya mazingira ya
mwaka 2004.
Kifungu hicho kinasema yeyote ambaye atachafua mazingira kwa namna
yoyote atachukuliwa hatua ikiwemo kufungiwa kiwanda pamoja na kulipa
faini.
Akizungumza na wanahabari wakati akikifungia kiwanda hicho,
Mwanasheria wa NEMC, Heche Suguta alisema wamepokea malalamiko mengi
kutoka kwa wakazi ambao wanakizunguka kiwanda hicho pamoja na
wafanyabiashara wadogo wadogo wakilalamikia vumbi hilo kuathiri afya.
Alisema baraza lilijulishwa kuwa uchafuzi unaofanywa na kiwanda
hicho umesababisha watoto kupata mafua yasiyoisha, kukohoa, kuumwa
vichwa na Kifua Kikuu (TB).
Walilalamikia wakati mwingine kushindwa kulala.
Heche alisema vumbi hilo ambalo ni la saruji limesababisha matatizo
mengi kwa wananchi na kwamba hawapo tayari kuona watu wakiendelea
kupata shida.
“Tumeamua kukifungia kiwanda hiki kikubwa cha Cement cha Tanzania
ili iwe fundisho kwa viwanda vingine ambavyo vina tabia ya kukaidi
maagizo ya serikali,” alisema Aliwaambia wanahabari kuwa endapo kiwanda
hicho kitakiuka agizo hilo polisi na NEMC watamkamata Mkurugenzi wake
na utaratibu mwingine wa kisheria utaendelea.
Alieleza kuwa kabla ya kukifungia kiwanda hicho jana walituma
wataalamu kwenda kuchunguza suala hilo ili kubaini hali ya
wanaathirika.
Wataalamu hao walithibitisha kuwa kiwanda hicho kinatoa vumbi lenye athari kiafya na hatua ya kukifungia ilichukuliwa.
Awali Mkurugenzi wa Twiga Cement , Alfonso Rodriguez, alisema bomba
ya kupitishia vumbi la saruji la kiwanda kipya limeharibika, hatua
iliyowalazimisha kutumia la kiwanda cha zamani ambalo limeelekezwa
angani.
Alisema kiwanda hicho kinafanya marekebisho ya kasoro hiyo.
-NIPASHE
Maoni
Chapisha Maoni