Sserunkuma ni habari nyingine
DANNY Sserunkuma ambaye ametua
Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya, leo atajikuta akishuka kwenye Uwanja wa
Mkwakwani, jijini hapa, huku akiwa na usongo zaidi wa kucheka na nyavu
kuthibitisha ubora wake mbele ya Mkenya, Rama Salim.
Mganda huyo na Salim walicheza
pamoja katika safu ya ushambuliaji ya Gor Mahia kwenye Ligi Kuu ya Kenya,
ambapo wawili hao walikuwa ni moto wa kuotea mbali katika kucheka na nyavu.
Kwa kiasi kikubwa, wawili hao ndio
waliotoa mchango mkubwa kwa Gor Mahia kutwaa ubingwa wa Kenya mara mbili
mfululizo, wakifunga mabao muhimu katika mechi za timu hiyo.

Lakini baada ya mambo ya kiuchumi
kwenda kombo kwenye kikosi hicho cha Kenya, Sserunkuma alijikuta akitua Simba
na Salim Coastal Union, japo walikuwa wakipendwa mno na wapenzi wa klabu hiyo.
Sserunkuma, ambaye alianza
kuitumikia Simba kwa kusuasua, tayari ameanza cheche zake, akiwa amefunga mabao
matatu katika mechi tatu za hivi karibuni za Ligi Kuu Bara.
Hali hiyo inaonekana kuanza kumjenga
kisaikolojia kumwezesha kuendeleza makali yake leo dhidi ya Coastal, kama
alivyokuwa Gor Mahia ambako aliibuka mfungaji bora wa ligi ya Kenya kwa misimu
miwili mfululizo.
Salim alizungumza na BINGWA jana
ambapo hakusita kueleza jinsi anavyofahamu uwezo wa kufunga mabao alionao
Sserunkuma, hivyo kujipanga kumkabili kwa tahadhari kubwa.
Alisema kuwa Sserunkuma ni
mshambuliaji mzuri, lakini pia ni mfungaji bora, hivyo amewatahadharisha mabeki
wao kumpa uangalizi wa hali ya juu leo.
“Hapa tulipo hatuweki vichwa chini
kutokana na kuuangalia mchezo huo kwa makini mno, tunahitaji kushinda na
tumejiandaa kwa hilo, kwani hatuwezi kukubali kupoteza mechi mbili kwenye uwanja
wetu wa nyumbani,” alisema.
Coastal Union
wanaivaa Simba leo ikiwa ni baada ya kufungwa bao 1-0 na Yanga katika mchezo wa
ligi hiyo Jumatano ya wiki hii Uwanja wa Mkwakwani.
Katika msimamo wa
ligi hiyo, Simba wapo nafasi ya 8, wakiwa na pointi 16 baada ya kushuka dimbani
mara 12, wakati Coastal Union wakishika nafasi ya saba kutokana na mechi 13,
wakiwa na pointi 17.-Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni