Simba yairuka kimanga Fifa
BAADA ya Simba kuagizwa kumlipa beki Donald Mosoti
takribani dola za Kimarekani 14,400 kwa kusitisha mkataba, klabu hiyo imesema
haijapokea barua yoyote inayowataka kufanya hivyo.

Simba ilimsainisha Mosoti mkataba wa miaka miwili na nusu akitokea
Gor Mahia ya Kenya, ambapo alicheza nusu msimu na kutupiwa virago vyake, ndipo
akaamua kupeleka madai yake Shrikisho la Soka Ulimwenguni, Fifa, kwa lengo la
kudai haki zake.
Juzi Fifa ilitoa uamuzi wa kuitaka klabu ya Simba kulipa
fedha hizo kwa muda wa siku 30 zijazo pamoja na riba ya asilimia tano ya malipo
yake kwa mujibu wa uamuzi uliofikiwa na majaji.
Katibu Mkuu wa Simba, Stephen
Ally, amesema bado hawajapokea barua kutoka Fifa inayoagiza kumlipa beki wao wa
zamani, hivyo watakapopata watatolea uamuzi na kuliweka bayana.
“Kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala hilo, bado hatujapewa
barua kutoka Fifa, hivyo tunasubiri barua na baada kuona inavyoeleza tutajua
nini cha kufanya,”
Simba walimtema Mosoti, ambaye alikuwa kipenzi cha
mashabiki kutokana na kiwango alichokionyesha kwa muda mfupi tangu kusajiliwa
kwake ili kupisha usajili wa Emmanuel Okwi, aliyekuwa akiichezea Yanga.
Maoni
Chapisha Maoni