Yanga ‘yaiovateki’ Simba
KASI ya mazoezi waliyoanza nayo Yanga ni wazi kwamba
‘wameiovateki’ Simba ambayo licha ya kuanza kambi muda mrefu lakini bado
inasuasua.
Kikosi cha Yanga kinaonekana kuja kivingine kutokana
na kufanya mazoezi makali na ya kasi tofauti na ilivyo kwa watani wao wa jadi,
Simba ambao bado wameweka mkazo katika mazoezi ya viungo katika ‘gym’ ya
Chang’ombe, Dar es Salaam.
Japo Simba wamekuwa wakianzia gym na kuhamia
uwanjani kwenye Uwanja wa TCC Chang’ombe, lakini mazoezi yao bado
hayajachanganya vizuri kwani kuna baadhi ya nyota wao wa kigeni, Waganda
Emmanuel Okwi na Joseph Owino hawajajiunga na wenzao.

Lakini kwa upande wa Yanga, kila kitu kinaonekana
kwenda sawa kwani nyota wao wote wa kigeni wameripoti, akikosekana mzawa mmoja
tu, Juma Kaseja ambaye hajulikani aliko.
Kwa kiasi kikubwa, ujio wa Mbrazil Emerson de
Oliveira Neves Roque, umeonekana kuzidi kuwachochea wachezaji wa Yanga kwani
hakuna anayetaka kuwa nyuma kuepuka kupoteza namba katika kikosi cha Mbrazil,
Marcio Maximo.
Katika mazoezi ya mwishoni mwa wiki na jana, Yanga
wameonekana kubadili mambo kadhaa ndani ya timu hiyo, ikiwamo kasi, mbinu,
mfumo na mengineyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa Nani Mtani Jembe
dhidi ya watani wao wa jadi, Simba utakaopigwa Desemba 13, mwaka huu.
Kwa maana hiyo, Yanga watavaana na Simba wakiwa
katika sura tofauti na ilivyokuwa walipopambana Oktoba 18, mwaka huu katika
mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na timu
hizo kutoka suluhu.
Katika mazoezi ya jana yaliyofanyika kwenye Uwanja
wa Shule ya Sekondari Loyola, Dar es Salaam, wachezaji wa Yanga wameonekana
kubadilika kuanza katika kasi, nidhamu ya mchezo na hata ufundi, huku wakiwa
makini katika kufuata maelekezo ya makocha wao.
Kwenye mazoezi hayo yaliyoanza saa 2:00 asubuhi,
Maximo na wasaidizi wake, Leonardo Neiva, Salvatory Edward, Juma Pondamali na
Shadrack Nsajigwa, walikuwa wakitilia mkazo zaidi namna ya kushambulia kwa
kasi.
Maximo aliwataka wachezaji kukimbia na kupigiana
mipira kupasha miili yao kabla ya kuanza rasmi programu yake ya siku.
Kocha huyo alianza rasmi programu yake kwa kuwapa
mbinu mbalimbali washambuliaji wake, Hamis Kiiza, Jerry Tegete, Mrisho Ngassa
na Said Bahanuzi jinsi ya kupanga mashambulizi na kufunga mabao kutokana na
krosi za mawinga wa pembeni.
Katika zoezi hilo, aliwagawa wachezaji katika
makundi matatu; mawinga, washambuliaji wa kati na mabeki na kuwataka mawinga wa
pembeni kupokea mipira kutoka viungo wa kati na kupiga krosi kuelekea kwa washambuliaji
wao.
Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite walitakiwa kuwapigia
pasi viungo wa pembeni, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho ambao walitakiwa kupiga
na hatimaye kuunganishwa na akina Bahanuzi, Tegete na Kiiza kumfunga kipa, Ally
Mustapha ‘Barthez’.
Zoezi hilo lililodumu kwa takribani dakika 45,
lilifanywa vema na wachezaji wa timu hiyo, akiwamo Emerson aliyeendelea
kuwaacha hoi wenzake kutokana na ‘mavituz’ yake adimu.
Baadaye Maximo aligawa vikosi viwili; cha kwanza kikiundwa
na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Jery Tegete,
Mrisho Ngassa na Simon Msuva, wakati kile cha pili kilikuwa na Ally Mustapha ‘Barthez’,
Salum Telela, Said Juma, Rajabu Zahir, Pato Ngonyani na Emerson.
Maximo alivitaka vikosi vyote viwili kucheza kwa
kufuata maagizo yake ambapo aliwapa mbinu za namna ya kushambulia kwa kasi, kukaba,
kupiga krosi na kumiliki mpira.
Zoezi hilo lilikuwa mahahusi kwa ajili ya kuwapa
mbinu wachezaji wake namna ya kucheza na kushambulia kwa kasi kisha mabeki
kusogea mbele kupanga mashambulizi wakati wakishambulia lango la timu pinzani.
Kwenye mazoezi hayo, kulishuhudiwa
vitu adimu kutoka kwa Emerson.
Pasi za uhakika (rula) na za visigino, vilikuwa
sehemu ya mbwembwe za kiungo huyo ambapo aliweza kupiga zaidi ya pasi tano
zilizomfikia winga, Mrisho Ngassa.
Emerson aliendelea kuonyesha uwezo wake mkubwa
ambapo aliweza kufungua vyumba na kupewa pasi kisha kupiga pasi kwa wenzake kwa
ajili ya kupandisha mashambulizi kwenye lango la timu pinzani.
Yanga kwa wiki ya pili mfululizo ipo katika mazoezi
makali kujiwinda na mpambano wake wa Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba
utakaopigwa Desemba 13 mwaka huu.
Maoni
Chapisha Maoni