Yanga yafanya usajili wa kutisha
YANGA imefanya
bonge la usajili ambao kama utakamilika ndani ya wiki hii, basi kikosi cha timu
hiyo kitakuwa moto wa kuotea mbali.
Wanajangwani hao
wamemalizana na kiungo mshambuliaji kutoka Brazil, Emerson De Oliveira Neves
Roque, baada ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja na sasa wanataka kufunga usajili
wao kwa kishindo kwa kumleta nchini bonge la straika lenye uwezo wa kutupia
mabao kila mara.
![]() |
Jonas Sakuwaha |
Taarifa za
uhakika kutoka kwa kigogo mmoja aliyepo kwenye masuala ya usajili zinasema
straika huyo atakuwa wa mwisho kusajiliwa katika kipindi hiki cha dirisha dogo
la usajili na pia atawasili ndani ya wiki hii kwa ajili ya kumalizana na
Wanajangwani hao.
Licha ya kwamba
benchi la ufundi la klabu hiyo bado limeficha jina la straika anayekuja, lakini walikuwa katika mazungumzo ya chini kwa chini na
mshambuliaji, Mohamed Traore kutoka Mali ambaye anaichezea El Merreikh ya
Sudan.
Mbali na Traore
ambaye anasifika kwa upachikaji wa mabao, mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu
Tanzania Bara, walikwenda mbali zaidi na kufanya mazungumzo na Mzambia Jonas
Sakuwaha anayeichezea TP Mazembe ambaye naye ni mkali wa mabao.
Kwa sasa baada
ya Yanga kumtema Mbrazil Geilson Santos ‘Jaja’ wamebakiwa na washambuliaji
wanne tegemeo ambao ni Hamis Kiiza, Jerryson Tegete, Husein Javu, pamoja na
Said Bahanuz na wanataka kuleta mtambo mwingine wa mabao.
Kama dili hilo
likifanikiwa ni wazi Mganda Hamis Kiiza hatakuwa na chake kwa Wanajangwani hao
kwani amekuwa akitajwa mara kwa mara kuondoka kutokana na kiwango chake
kutowaridhisha mabosi wake licha ya kwamba hata Niyonzima naye anahusishwa na
kutakiwa na Simba na Azam.
Yanga mpaka sasa
inao wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka
nchini (TFF), ambao ni Niyonzima, Mbuyu Twite, Andrey Coutinho, Emerson, pamoja
na Kiiza ambaye ndiye yupo kwenye mstari mwekundu.
Katika safu hiyo
ya ushambuliaji ya Yanga hadi Ligi Kuu inafikia raundi ya saba ni Tegete peke
yake ambaye alifanikiwa kupata mabao mawili aliyoyafunga katika mchezo dhidi ya
Stand United, huku Javu, Kiiza pamoja na Bahanuzi wakiambulia patupu wakati
winga Simon Msuva akiwa kinara kutokana na mabao yake matatu.
Kutokana na
ukweli huo ndiyo maana uongozi na benchi la ufundi wakaamua kutafuta straika
mmoja mwenye uwezo wa kucheka na nyavu hasa ikizingatiwa kuwa lengo lao kubwa
ni kuhakikisha wanarejesha ubingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara waliopokwa
na Azam msimu uliopita.
Mbali na
kujipanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Wanajangwani hao wanataka kufika mbali
katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika mwakani
ambapo wao ndiyo watakaoiwakilisha nchi, huku Azam wakishiriki Ligi ya Mabingwa
Barani Afrika baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita.
Msimu uliopita
Yanga walikuwa na washambuliaji wakali kama Didier Kavumbagu ambaye alikuwa
kinara wa ufungaji kwa upande wa Wanajangwani hao kabla ya kuamua kutimkia Azam
ambapo kwa sasa anaongoza akiwa na mabao manne sawa na Dany Mrwanda wa Polisi
Morogoro, Ame Ally wa Mtibwa Sugar, pamoja na Rahma Salim wa Coastal Union.
Katika dirisha
dogo la msimu uliopita waliamua kuongeza nguvu kwenye safu hiyo ya usajili
baada ya kumuongeza Emmanuel Okwi ambaye hata hivyo hakudumu kwa muda mrefu
kutokana na kutofautiana na uongozi katika suala zima la malipo na msimu huu
kuamua kurejea Simba.-Dimba
Maoni
Chapisha Maoni