Watendaji waswekwa rumande
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magessa Mulongo, ameanza kazi kwa
kuwaweka rumande baadhi ya madiwani na watendaji wa
halmashauri za wilaya kutokana na kutofautina kauli ndani ya vikao.
Mulongo
alikabidhiwa ofisi Novemba 25 mwaka huu
akitokea Arusha. Amekwisha kuwatangazia
viongozi wa jiji la Mwanza kuwa hatafanya kazi na watumishi wazembe
wanaoendekeza porojo za siasa badala ya vitendo.
Katika
kikao cha kwanza kilichohusisha mameya, wakurugenzi wa halmashauri zote,
wakuu wa idara, wakuu wa wilaya na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa,
aliwaamuru mameya na wakurugenzi wa halmshauri kueleza sababu za Jiji la Mwanza
kupata hati chafu na akataka
ripoti ya utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete la ujenzi wa maabara.
Baada ya maelezo ya viongozi hao, RC Mulongo
amesema anasikitishwa kwa kitendo cha viongozi wa mkoa huo
kumdanganya kwa kumpatia taarifa ya
maandishi ambayo haina uwiano na maelezo yao na kuwaita kuwa ni viongozi
mfilisi walioagana na Serikali.
“Nimegundua taarifa niliyokabidhiwa ya kila wilaya ni
ya uongo kwa sababu ukweli nimeujua hapa kwa maelezo yenu; kwanza majibu yenu
ni ya siasa, hayajitoshelezi, nimegundua viongozi wengi wanaligharimu taifa na
wengine hawajui wajibu wa nafasi zao.
“Hakuna mtu anayefanya kazi ya mwingine wakati mwenyewe
yupo, sitaki visingizio katika utekelezaji wa majukumu anayeona haendani na
kasi aondoke mapema, sitaki hati chafu tena, pia naomba wakurugenzi na
watumishi wengine sitaki fujo,wengi wenu nimeambiwa mnayo miradi binafsi wananchi
wanateseka wakati nyie mnacheka,”.
Mulongo ambaye alianza ziara ya kutembelea wilaya
Novemba 2, ikiwa ni siku ya pili tangu kukabidhiwa ofisi hiyo na kuanzi
Wilaya ya Misungwi ambako aliingia
mgogoro na watendaji wawili ndani ya kikao baada ya kutofautiana kauli
kuhusu ujenzi wa maabara kitendo kilichosababisha kuagiza kukamatwa na kuwekwa
rumande.
Pia Mulongo amehitilafiana na Diwani wa Chadema Kata ya
Mbungani Wilaya ya Nyamagana, Hassan Kijuu, ambaye alimtaka mkuu huyo kutokuwa
mbabe na kutowafanya kama watoto na badala yake anatakiwa kuheshimiana katika
kazi.
Mulongo alizidi kukasirishwa na diwani huyo baada ya
kumweleza kuwa hakuzingatia muda wa kikao kilichoanza saa 3.00 asubuhi lakini
yeye aliingia saa 6.00 mchana.
RC aliingia mgogoro mwingine na watendaji na madiwani wilayani Ukerewe
juzi na kuagiza askari kumkamata diwani wa Chadema na kumuweka rumande
baada ya kutofautiana kauli juu ya ujenzi wa maabara.
Kutokana na migogoro hiyo, hivi sasa Rc Mulongo
anatembea na askari wawili wa ulinzi na wakati mwingine kuongozwa na pikipiki za ving’ora
kwa kile kinachoelezwa ni kuhofia usalama wake.
Maoni
Chapisha Maoni