Wanne mbaroni kwa mauaji
JESHI la
Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wanne wanaodaiwa kujihusisha na
uchochezi wa vurugu na mapigano ya jamii
ya wafugaji yalitokea Novemba 26 katika Kijiji cha Kihale Tarafa ya Chole wilayani
Kisarawe na kusababisha mauaji ya watu tisa.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, ametoa ufafanuzi huo alipozungumza
na waandishi wa habari kuhusiana na
tukio la mapigano ya wafugaji Wasukuma na Wabarbeig.

Matei amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Chacha Mganja (24), Kidaini Kidatu (20), Musa Bohai (20)
na Emmanuel Kihuga (29) ambao kwa
pamoja wanadaiwa kuwa chanzo cha mapigano hayo.
Amesema
pamoja na kukamatwa kwa watuhumiwa hao lakini bado Jeshi hilo linaendelea na
msako mkali wa kuhakikisha wengine waliohusika katika tukio hilo wanatiwa
nguvuni lengo likiwa ni kutaka kuimarisha usalama wa maeneo husika na hata
kudhibiti vitendo hivyo visitokee maeneo mengine.
Matei
amesema mpaka sasa watu sita waliouawa katika mapigano
hayo wametambuliwa na tayari madaktari wamewafanyia uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa mazishi. Hao ni Sarafu Samson (18), Njili Juma (20), Kajilo
Naelomi (27), Daniel Nyerere (30), Pascal Matias na Alex Kiteu (21).
“Mapigano
hayo yalitokea Novemba 26 asubuhi katika Kijiji cha Kihale baada ya Alex Kiteu
ambaye ni Mbarbeig kuiba ng’ombe 51 mali ya Doto Charles. Katika
msako Kiteu alikutwa akiwa na ng’ombe hao na hivyo Wasukuma wakamuua kwa
kutumia mapanga, mikuki na mishale,”
Amesema
baada ya Wabarbeig kuona mwenzao ameuawa siku ya pili walilipiza kisasi kwa
kutumia mishale, mikuki na mapanga kufanya mashambulio na kuwaua Wasukuma ambao
inadaiwa walikuwa sita .
Kutokana
na mapigano hayo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantum Mahiza, amewataka
wafugaji walioingia mkoani Pwani bila
kufuata utaratibu waondoke haraka na kama watashindwa kufuata maagizo yake
watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali za sheria.
Maoni
Chapisha Maoni