Simba yawaanika wauaji wa Express
MSHAMBULIAJI mpya wa timu ya Simba, Mganda Dan
Sserunkuma leo anatarajia kuongoza mashambulizi ya timu hiyo itakapovaana na
Express ya Uganda.
Sserunkuma alitua nchini juzi na tayari amesaini
mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo, akitokea Gor Mahia ya Kenya
aliyomaliza nayo mkataba.

Mganda huyo ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu
Kenya msimu uliopita kwa mabao 16, ni tegemeo jipya la ushambuliaji kwenye
kikosi hicho akisaidiana na Mganda mwenzake Emmanuel Okwi.
Mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam unatarajia kuanza majira ya saa 11 jioni.
Kocha mkuu wa Simba, Patrick Phiri atautumia mchezo
huo kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga Desemba
13, mwaka huu.
Express inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa
Ligi Kuu nchini Uganda, tayari imeshatua nchini kwa ajili ya mchezo huo na ule
wa Yanga itakayopambana nayo kesho.
Wachezaji wapya wa Simba ambao nao huenda wakawemo
kwenye mchezo huo ni mshambuliaji Danny Mrwanda, aliyetokea Polisi Morogoro,
huku kiungo Omar Mboob naye akitarajia kujaribiwa.
Mboob raia wa Gambia yupo kwenye majaribio ndani ya
kikosi hicho tokea mwanzoni mwa wiki hii, hiyo ni baada ya Phiri kupendekeza
atafutwe kiungo wa kuongeza nguvu katika kikosi hicho.
Simba iliyoanza vibaya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara kwa kuambulia ushindi wa mchezo mmoja na sare sita, ipo kwenye mawindo ya
kuimarisha kikosi chake ambapo kwa sasa inafukuzia kipa, kiungo na beki wa
kati.
Kipa anayedaiwa kuwa mbioni kujiunga na wekundu hao
ni kipa wa zamani wa timu hiyo, Juma Kaseja aliyegoma kurejea kwenye timu yake
ya Yanga baada ya kutofautiana na uongozi.
Maoni
Chapisha Maoni