Muhuri wawaponza wagombea Chadema


Wagombea hao 1,400 kutoka vijiji 56 vya jimbo hilo, walikutwa na dhahama hiyo baada ya kuwekewa pingamizi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya muhuri waliotumia katika fomu za uteuzi wa wagombea kusomeka ‘CDM’ badala ya Chadema kama ilivyozoeleka.

MUHURI mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umewaponza wagombea wake wote wa Serikali za Mitaa wa Jimbo la Meatu, mkoani Shinyanga.
Pamoja na chama hicho kukata rufaa, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Meatu, alitupilia mbali rufaa hiyo hali iliyozua vurugu kutoka kwa wanachama wa Chadema waliotaka mwenyekiti huyo kuwasomea rufaa hiyo, badala ya kuwapa barua wakasome wenyewe kama alivyofanya.
Hatua hiyo ilisababisha polisi kuwakamata Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Wilaya (Bavicha) na viongozi wengine nane.
Mbunge wa Meatu, Meshack Opurukwa (Chadema), alisema kilichofanywa na kamati ya rufaa ni uonevu, kwani walioweka pingamizi si wagombea kama sheria zinavyosema.
“Pingamizi lile ni batili kwa sababu waliokata rufaa ni wanachama, si wagombea na wanaposema muhuri ule si wetu wanamaanisha nini? Wa kulalamika kuhusu uhalali wa muhuri ni sisi, si Serikali wala mtu mwingine yeyote.
“Hatua hii imesababisha wagombea wa CCM wanaowalinda kupita bila kupingwa na sisi hatutakuwa na Serikali katika ngazi ya mtaa jambo ambalo si haki kwa sababu walijua tutashinda kwa kishindo,” alisema Opurukwa.
Akizungumzia sakata hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema chama chao kimewekewa mapingamizi mengi, lakini batili jambo linalompa hofu kwamba kamati za rufaa zinatekeleza maagizo waliyopewa kukiondoa chama hicho katika Serikali za mitaa.
Alisema hatua ya kukataa rufaa za mapingamizi yanayowekwa ni kufanya mlolongo uwe mrefu ili wakasirike na kwenda mahakamani ambako itachukua muda mrefu kutolewa uamuzi jambo ambalo Chadema wanalipinga.
“Si Meatu tu, tumewekewa pingamizi 500 Karagwe, hizi sababu zake ni wadhamini, Mwanza 400 na Dar es Salaam 50, hii kwa Chadema haikubaliki sababu ya muhuri ni hoja isiyo na mashiko,”.-Mtanzania

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4