Miaka 60 jela kwa kutorosha twiga
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro leo imemhukumu miaka 60 jela, mshitakiwa wa kwanza raia wa Pakistani, Kamran Ahmed na
kuwaachia huru Watanzania watatu katika kesi ya utoroshaji wanyama hai 153
wakiwemo twiga wanne.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Simon Kobelo,
amesema baada ya upande wa jamhuri kufanikiwa kujenga kesi dhidi ya Mpakistani
huyo kwa kiwango kisicho na shaka, mahakama hiyo imeridhika kwamba alitenda makosa
yote manne yaliyowasilishwa dhidi yake.

Kobelo amedai mahakama hiyo pia inaawachia huru Watanzania
watatu, Hawa Mang’unyuka, Mathew Kimathi na Michael Mrutu kwa sababu upande wa
jamhuri imeshindwa kujenga kesi dhidi yao na hata ushahidi uliowasilishwa hauoneshi
kuwaunganisha washitakiwa hao moja kwa moja na kosa la kusafirisha wanyama hai
nje ya nchi.
Katika hukumu hiyo, Kamran, alikutwa na makosa manne,
kushiriki na kula njama ya kutenda uhalifu kinyume cha kifungu 57 (1), sehemu
ya 4(1), sura ya kwanza ya kosa la uhujumu uchumi na kushiriki utoroshaji wa
wanyama hai wenye thamani ya Sh 170, 575,500.
Kosa la pili ni kufanya biashara ya kukamata na kusafirisha
wanyama hai wakiwemo twiga, chui, ndege wa aina mbalimbali, duma, nyati, pofu,
pundamilia na swala bila leseni.
Kosa la tatu ni kukutwa na nyara za Serikali katika Uwanja
wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), tukio lililotokea Novemba 26, 2010 na kosa
la nne ni kuisababishia Serikali hasara ya Dola 113.7 za Marekani kwa kufanya
biashara kinyume cha sheria.
Kuhusu kumuachia huru mshitkakiwa namba mbili, Hawa ambaye
ni mmiliki wa Kampuni ya Harm Marketing na Luwego Bird Trappers inayodaiwa
leseni yake kutumika kuhalalisha ukamataji na utoroshaji huo.
Hakimu Kobelo alidai kwa mujibu wa vielelezo vilivyowasilishwa
ni wazi kwamba Harm ilipewa kibali halali cha kukamata wanyama hai na mamlaka
husika hivyo mahakama hiyo inashindwa kumtuhumu moja kwa moja na utoroshaji
huo.
“Ukirudi kwa mshitakiwa wa pili, jibu liko wazi, Hawa
kupitia kampuni yake ya Harm Marketing alikuwa na leseni za kufanya biashara ya
kukamata wanyama, baadaye kupitia mamlaka hizo hizo ziliruhusu mshitakiwa wa
kwanza kufanya biashara hiyo hiyo kupitia Harm Marketing na katika kipindi
hicho, Kamran aliendelea kutumia leseni hiyo mara kwa mara,” Kobelo.
Kwa upande wao, washitakiwa wa tatu na nne, Mathew na
Michael kwa sababu hakuna sehemu yoyote inayoonesha ushiriki wao katika
utoroshaji zaidi kutekeleza wajibu wao kama walivyoekezwa na wakuu wao wa kazi
kipindi hicho.
Novemba 26, 2010, Kamran anadaiwa kuwatorosha wanyamka hai
153 wakiwemo twiga wanne kwenda Doha nchini Qatar kupitia KIA kutumia ndege ya
jeshi namba C17, kinyume cha kifungu namba 84(1) cha Sheria namba tano ya Uhifadhi
wa Wanyamapori ya mwaka 2009.
Maoni
Chapisha Maoni