Mgombea CCM mbaroni kwa rushwa
TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), inamshikilia kada wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Mwangwa Ephraim, kwa madai ya kupokea rushwa na kushindwa
kurudisha fomu.
Kada
huyo, alichukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kitongoji
cha Kitagula, Kijiji cha Bumangi wilayani Butiama, lakini alishindwa kurudisha
fomu yake Novemba 23, mwaka huu saa 10:30 kama ilivyopangwa.
Akizungumzia
sakata hilo, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mara, Holle Makungu, alisema kada huyo
anadaiwa kupokea rushwa ya Sh 100,000 kutoka kwa mgombea mwenzake (jina
linahifadhiwa) ili asirudishe fomu kwa muda uliopangwa ili mpinzani wake huyo
apite bila kupingwa.
Makungu amesema uchunguzi uliofanywa na Takukuru unaonyesha kuwapo mazingira ya rushwa.
Mgombea huyo aliyepitishwa na chama chake, wakati wa kurudisha fomu ulipofika
alizima simu ili kupoteza mawasiliano kwa viongozi wake hadi muda wa kurudisha
fomu ulipomalizika.
“Tumefanya
uchunguzi na kubaini mtuhumiwa alipokea rushwa kiasi cha Sh 100,000 kutoka kwa
wakala wa mshindani wake toka chama shindani kwenye eneo hilo ili mgombea wake
apite bila kupingwa.
“Kitendo
hiki ni kinyume cha sheria na kinadumaza demokrasia ya vyama vingi, kwa kutumia
rushwa kunawaondoa wagombea ambao wamepewa dhamana na vyama vyao,”
Makungu.
Hata
hivyo, alisema uchunguzi zaidi wa tuhuma hizo bado unaendelea na mara
utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.
Maoni
Chapisha Maoni