Meno ya tembo yamburuza kortini
MKAZI wa
kijiji cha Lamadi wilayani Busega,
Madeni Nindwa (62), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Magu akikabiliwa
na mashitaka ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni
17.3 kinyume cha sheria.
Wakili
wa Serikali Mfawidhi wa Mkoa wa Simiyu, Yamiko Mlekano pamoja na Mwanasheria wa
Tanapa, Emmanuel Zumba, wamedai mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Magu,
Robert Masige, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Novemba
26 mwaka huu. 

Mtuhumiwa anakabiliwa
na mashitaka mawili ya kumiliki nyara za
serikali ambazo ni meno ya tembo yenye thamani ya Sh 17,325,000 na
kufanya biashara hiyo kinyume cha sheria.
Zumba amedai
mtuhumiwa alikamatwa Novemba 26 mwaka huu nyumbani kwa rafiki yake katika mji mdogo wa
Lamadi wilayani Busega.
Alidai mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na vipande
sita vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 18 vikiwa vimehifadhiwa kwenye
mfuko pamoja na mzani mmoja wa kupimia
meno hayo.
Zumba
alisema mashahidi watakuwa tisa na
upelelezi umekwisha kukamilika.
Mtuhumiwa
huyo aliyakana mashtaka yake na kupelekwa rumande hadi Desemba 8 mwaka huu kesi yake
itakapotajwa tena.
Maoni
Chapisha Maoni