Mboob kiboko ya Emerson
KIUNGO mpya wa Simba, Mgambia Omar Mboob, ameanza
kwa kukiona cha moto baada ya kuhenyeshwa vilivyo katika mazoezi ya jana,
akiandaliwa kumfunika Mbrazil, Emerson de Oliveira Neves Roque wa Yanga,
aliyesaini mkataba wa kuichezea timu hiyo jana.
Mboob akiwa na wachezaji wenzake wa Simba, walianza
mazoezi ya viungo katika ‘gym’ ya Chang’ombe, Dar es Salaam kabla ya kuhamia ya
uwanjani kwenye Uwanja wa TCC Chang’ombe, jijini.
Katika mazoezi hayo ya gym, wachezaji hao
walihenyeshwa vilivyo na kujikuta wakiwa hoi na hatimaye kwenda kunyoosha
viungo vyao uwanjani kwa kukimbia na kuchezea mpira.
kawaida tu.
Usajili wa Mboob umetafsiriwa kama sehemu ya Simba
kujibu mapigo ya Yanga waliomsajili kiungo Emerson ambaye vipande vya video
vinamwonyesha kama mchezaji aliyekamilika kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki
mpira, kukaba, kupora mipira, kupiga pasi murua, kufunga na mengineyo kama hayo.
Iwapo Mgambia huyo atafuzu, atailazimisha Simba
kufyeka mchezaji mmoja wa kimataifa kati ya Amis Tambwe na Pierre Kwizera wote
raia wa Burundi.
Mbali ya Kwizera, Simba ina viungo mahiri kama Said
Ndemla, Shaaban Kisiga, Wiliam Lucian ‘Gallas’ na Jonas Mkude.
Katika hatua nyingine, Simba imezidi kufanya kweli
baada ya kumnasa msaidizi wa Mganda, Joseph Owino katika nafasi ya ulinzi wa
kati, ambaye ni beki kisiki wa Mtibwa Sugar, Salim Mbonde.
Tangu kuondoka kwa Mkenya Donald Mosoti ambaye
alikuwa akishirikiana vema na Owino, Wekundu wa Msimbazi hao wamekuwa katika
wakati mgumu kutokana na safu ya ulinzi wa kati kupwaya.
Isihaka Hassan aliyekuwa akisaidiana na Owino,
ameonekana kukosa uzoefu hali iliyotoa mwanya kwa timu pinzani kuipenya safu
hiyo.
Simba wamekuwa wakimfukuzia Mbonde kwa muda mrefu
kutokana na aina yake ya uchezaji ambapo ameisaidia Mtibwa kuwa kileleni katika
msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakiwa na pointi 15.
Taarifa za uhakika kutoka kwa mmoja wa vigogo wa
Simba anayeunda Kamati ya Usajili, zinadai kuwa mazungumzo kati ya pande hizo
mbili yamefikia mahala pazuri na muda wowote beki huyo atalamba mkataba wa
miaka miwili.
“Kwa kweli tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana
kuhakikisha tunaboresha kikosi chetu, baada ya kufanya hayo kwa Dan Sserunkuma
na kufanikiwa kumnasa, hatimaye Mbonde naye ameingia kwenye anga zetu na muda
wowote kuanzia sasa tutaingia naye mkataba,” alisema kigogo huyo.
Alisema lengo la kumsajili Mbonde ni kusaidiana na
nahodha wao, Owino ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa ambapo kwa sasa atapata
ahueni kutokana na uwezo wa beki huyo wa Wakata Miwa na kwamba amewataka
mashabiki wa Simba kutokuwa na wasiwasi wowote juu ya kikosi chao.
Kabla ya Mbonde kutua Mtibwa, aliwahi kufanya
majaribio Simba kuelekea msimu uliopita wakati huo timu ikiwa chini ya Kocha
Mkuu, Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, lakini
alionekana si chochote na kuamua kutimkia Manungu, Turiani.
Tangu kutua kwake Mtibwa, amekuwa lulu na sasa Simba
wamefanya kila linalowezekana kunasa saini yake.
Msimu huu, Mbone alionekana zaidi katika mtanange wa
ufunguzi wa Ligi Kuu Bara wakati Mtibwa walipokutana na Yanga ambapo Wakata
Miwa hao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku Mbonde akiwazuia vilivyo
washambuliaji wa Yanga waliokuwa chini ya Mbrazil, Geilson Santos ‘Jaja’ ambaye
amejiengua katika kikosi hicho cha Jangwani.
Mbonde aliendeleza ubabe wake kwa wakongwe wa soka
nchini walipomenyana na Simba ambapo aliwadhibiti vilivyo straika wa Wekundu wa
Msimbazi hao, wakiongozwa na Mganda, Emmanuel Okwi pamoja na Elias Maguli na
mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.-Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni