Mbaroni kwa kumnyonga mtoto
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro,
linamshikilia Zamir Shaban (27), mkazi wa eneo la Mkindo, Wilaya ya
Mvomero kwa tuhuma za kumnyonga hadi kufa mtoto wake wa kambo
mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Akizungumza na waandishi
wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Morogoro, Leonald Paul, alisema mauaji hayo yalifanyika Desemba 2 mwaka huu.

Alisema kwamba, mtuhumiwa huyo
ambaye alikuwa mume wa mama wa mtoto huyo, Rehema Mustafa,
inasemekana alimnyonga mtoto huyo kutokana na ugomvi wa kifamilia waliokuwa
nao.
“Inasemekana kulikuwa na ugomvi kati
yao uliopelekea mwanamke huyo kutafuta mume mwingine.
“Wakati wa mauaji hayo, mama wa
mtoto huyo alikuwa amekwenda dukani kununua vitu na alimwacha mtoto wake huyo
chumbani akiwa amelala.
“Mwanamke huyo aliporudi alimkuta
mtoto wake akiwa amelegea na alipotoa taarifa polisi,
mtuhumiwa alikamatwa na alipohojiwa alikiri kumnyonga mtoto
huyo kutokana na mgogoro uliokuwapo kati yake na mkewe,” alisema Kamanda Paul.
Kutokana na hali hiyo, alisema mtuhumiwa
ataendelea kuwa rumande hadi atakapofikishwa mahakamani baada ya taratibu za
kisheria kukamilika.
Maoni
Chapisha Maoni