Maximo aongeza dozi Yanga
KOCHA Mkuu wa
Yanga Mbrazil, Marcio Maximo,ameamua kutoa ‘full’ dozi ya mazoezi ya
kikosi chake kwa kuwaita pembeni kwa mafungu wachezaji wake na kuwaambia waache
masihara kwani ndio wanaotegemewa kuibeba timu hiyo.
Yanga inaendelea
na mazoezi katika Shule ya Sekondari Loyola jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya
kujiandaa na mechi zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na zile
za Nani Mtani Jembe.
Jana Maximo
alianza kuwaita 'chemba' mastraika wa timu hiyo; Jerryson Tegete, Said Bahanuzi
pamoja na Hamis Kiiza na kuwapa darasa kabla ya kuhamia katika idara nyingine.
Mbali na hilo,
kocha huyo pia aliamua kupanga kabisa wachezaji wa kupiga penalti na wale
watakaokuwa na jukumu la kupiga mipira ya faulo katika mazoezi ambayo
yalifanyika Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola jijini Dar es Salaam.
Maximo anajua
kwamba anakabiliwa na mchezo mgumu wa Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba Desemba
13 mwaka huu Uwanja wa Taifa ambapo hataki kufanya makosa yaliyofanywa na Ernie
Brandts, aliyekuwa kocha wa Wanajangwani hao walipokubali kichapo cha mabao 3-1
msimu uliopita katika mchezo kama huo.
Katika mazoezi
hayo Maximo alianza kuwapa wachezaji wake mazoezi ya kupasha moto misuli na
baadaye kuwafundisha namna ya kuunganisha krosi, zoezi lililofanywa na
wachezaji kwa ustadi mkubwa.
Baada ya Mbrazil
huyo kuridhika na zoezi hilo aliamua kugawa vikosi viwili ambapo cha kwanza
kiliongozwa na Deogratius Munish 'Dida,' Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin
Yondani, Nadir Haroub 'Cannavaro,' Haruna Niyonzima, Simoin Msuva, Andrey
Coutinho, pamoja na Jerryson Tegete.
Kikosi cha pili
langoni alisimama Aly Mustafa 'Barthez,' Salim Telela, Omega Seme, Rajab Zahir,
Emerson De Oliveira, Mrisho Ngassa, Hasan Dilunga, Nizar Khalfani, Said
Bahanuzi, pamoja na Mganda Hamis Kiiza.
Wachezaji hao
walionyesha kandanda la kuvutia kutokana na maelekezo ya kocha wao ambapo hadi
yanamalizika timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1, bao la kikosi cha
kwanza lilifungwa na Msuva na la kikosi cha pili likifungwa na Said Bahanuzi.
Baada ya
kumalizika zoezi la kucheza mpira ndipo likaja zoezi la upigaji penalti ambapo
waliopewa jukumu hilo walikuwa ni Cannavaro, Joshua, Msuva, Tegete, Bahanuzi,
Ngassa, pamoja na Kiiza ambapo Cannavaro na Msuva walionekana kung’ara kutokana
na kupiga penalti zao kiufundi zaidi.
Wakati wachezaji
hao wakipewa jukumu hilo lililosimamiwa na Maximo, kwa upande mwingine kocha
msaidizi Leonardo Neiva alikuwa akisimamia wale waliochaguliwa maalumu kwa
ajili ya upigaji faulo ambao ni Haruna Niyonzima, Andrey Coutinho, pamoja na
Nizar Khalfani huku Niyonzima akiibuka shujaa kwa kupiga kiufundi.
Walipofika
tamati ya mazoezi yote ndipo Maximo akawaita Tegete, Bahanuzi, pamoja na Kiiza
ambao ndio washambuliaji wa kutegemewa wa timu hiyo na kuafanya nao mazungumzo
yaliyodumu kwa dakika sita kabla ya kuwaruhusu kuondoka.
Yanga wanataka
kulipiza kisasi cha kufungwa mabao 3-1 na Simba Nani Mtani Jembe ya msimu
uliopita, ambapo msimu huu mchezo huo utachezwa Desemba 13 Uwanja wa Taifa na
kama timu hizo zikitoka sare itabidi kupigiana penalti hadi mshindi apatikane,
zoezi ambalo Maximo ameanza kulifanyia kazi.
Maoni
Chapisha Maoni