Hamis Kiiza aipasua Yanga
VIONGOZI wa klabu ya Yanga wamejikuta katika wakati
mgumu kufuatia kuvutana juu ya kuachwa kwa mshambuliaji wake wa kimataifa
kutoka Uganda, Hamis Kiiza.
Hamis Kiiza |
Hii ni mara ya pili kwa Kiiza kuwekwa kikaangoni kwa
kutaka kuachwa kwani katika kipindi kilichopita cha usajili aliponea
chupuchupu.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa, Kamati ya Usajili ililazimika kuitisha kikao
cha dharura kujadili suala la mchezaji
huyo.
Chanzo hicho kilisema kumeibuka mgawanyiko mkubwa
baina ya viongozi wanaounda kamati hiyo, ambapo wengine wametoa mapendekezo ya
mchezaji huyo kuvumiliwa hadi msimu huu wa ligi umalizike.
“Ni mara ya pili Kiiza kuleta mgawanyiko kwa
viongozi, kipindi cha nyuma wakati anataka kuachwa hali ilikuwa hivi na mwisho
wake alibaki kuitumikia timu hii,” kilisema chanzo hicho.
Kamati hiyo inayoongozwa na Seif Magari ilipingana
vikali, huku wengine wakidai mshambuliaji huyo kiwango chake kimeshuka hivyo ni
vizuri nafasi yake ikachukuliwa na mtu mwingine.
“Wengine wanadai kiwango cha Kiiza kimeshuka ila
wapo wanaomtetea na kusema hastahili kuondolewa kipindi hiki, kwani amekuwa na
mchango mkubwa wa timu hiyo,” alisema.
Chanzo hicho kilieleza kamati hiyo imeridhia
kukutana upya na kujadili suala hilo kabla ya Jumatatu, ili kuhakikisha masuala
ya usajili yanakamilika Desemba 14.
Habari za kamati hiyo kupanga kusajili mchezaji mpya
Mohamed Traore kutoka Mali zimezidi kushika kasi, huku timu ikiwa na jumla ya
wachezaji watano wa kimataifa.
Kiiza ambaye aliponea katika tundu la sindano
kutemwa na klabu hiyo, amebakisha miezi
sita kabla ya mkataba wake kufikia tamati.
Maoni
Chapisha Maoni