9 wauawa mapigano ya wafugaji Kisarawe

Kisarawe



WATU tisa wamefariki dunia katika Kijiji cha Kihale wilayani Kisarawe Pwani, baada ya kuibuka mapigano makali kati ya wafugaji wa jamii ya  Kisukuma na Wabarbeigi.
Tukio hilo lilitokea Novemba 26, mwaka huu ambapo inadaiwa chanzo cha mapigano hayo ni kijana wa Kibarbeigi kuuawa na vijana wa Kisukuma kwa madai ya wizi wa ng’ombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba hadi jana maiti zote hazijatambuliwa kwa majina.
Alisema uchunguzi wa kina unaendelea kutambua watu hao walikuwa wanaishi wapi.
“Chanzo cha mapigano haya kilianza wakati mtu mmoja ambaye ni Mbarbeigi  alipoiba mifugo kwa Msukuma mmoja. Hali hii ilisababisha mtu aliyeibiwa kuwapigia simu wenzake ambao walikusanyika na kuanza kumtafuta mwizi.
Alisema baada ya kumpata mwizi walimpiga hadi kufariki dunia jambo ambalo lilionyesha kuwapandisha hasira Wabarbeigi.
“Baada ya kuona mwenzao ameua waliamua kujibu mashambulizi dhidi ya Wasukuma ili kulipiza kisasi… hali hii ilisababisha amani kutoweka ambapo watu walikimbia ovyo kwa ajili ya kujiokoa,” alisema Kamanda Matei.
Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani, ilifanya juhudi za kukutana  na wafugaji wa jamii ya Wasukuma, Wamasai na Wabarbeigi ili  kuhakikisha wanasaidiana kuwasaka wahusika.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alisema amesikitishwa na kitendo hicho.
Kutokana na hali hiyo, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka wale wote waliohusika na kuwatia nguvuni.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM), alisema mauaji hayo ni mabaya na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuchukua hatua haraka za kuwasaka wale wote walichochea vurugu hizo.
“Nitashirikiana na Jeshi la Polisi na wananchi kuhakikisha tunarejesha amani, umoja na utulivu katika vijiji husika,” alisema Jafo.-Mtanzania

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4