Usajili mpya wa Simba
KAMA ulitegemea kwamba Patrick Phiri
anapigwa chini pale Simba umekosea. Tulia hapohapo usikie anachosema
kiongozi mkuu wa Simba, Rais Evans Aveva.
Amesisitiza kuwa hatamfukuza kocha huyo Mzambia na
tayari amempa uhuru wa kuchagua wachezaji anaotaka kuwasajili kwenye
dirisha dogo kwa gharama yoyote ile.
Mbali na hilo pia amempa uhuru wa kuchagua wapi
timu ikaweke kambi pamoja na mechi za kirafiki anazotaka kucheza wakati
huu wa mapumziko ambapo usajili wa dirisha dogo utaanza Novemba 15 hadi
Desemba 15.
Aveva ameliambia Mwanaspoti kuwa mashabiki wengi
hawakuelewa juu ya taarifa ya kumpa mechi mbili kocha Phiri haikuwa
kumfukuza bali ni kuwaandalia taarifa ya kipi ameona ni tatizo na
kupelekea timu yao kupata matokeo hayo ya sare mfululizo.
“Hatuwezi kumfukuza kocha kwa matokeo hayo,
tulimaanisha kwamba atuandalie ripoti ya kwa nini timu inapata matokeo
haya na nini kifanyike, lakini pia tumempa uhuru wa kupendekeza majina
ya wachezaji aliowaona kwenye ligi na anataka kuwasajili,” alisema.
“Hiyo iwe kwa wachezaji wa ndani na nje na kwa
nafasi anazotaka yeye bila kujali gharama, tumempa uhuru wa kupendekeza
timu iweke wapi kambi pamoja na mechi za kirafiki, hivyo mpango wa
kumfukuza Phiri haupo.”
Phiri aliwahi kuliambia Mwanaspoti kuwa anahitaji
kufanya marekebisho machache katika kikosi chake ambapo alitaja kuwa
anahitaji straika, kiungo mkabaji, kipa, mabeki wa pembeni (kulia na
kushoto) na beki wa kati.
Kila nafasi anahitaji mchezaji mmoja mmoja.
“Tukimaliza mechi ya Jumapili nitawakabidhi ripoti
viongozi wangu ambayo itaambatana na mapendekezo yangu ya usajili,
ambapo wao watatakiwa kuyafanyia kazi, sihitaji kusajili wachezaji wengi
kwani tutakuwa kama tunaanza upya kujenga timu, nitaangalia nafasi
zenye mapungufu,” alisema.
Baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wamedai kwamba kocha huyo ni mpole sana kiasi cha kufanya baadhi yao wamwingilie kwenye uamuzi.-Mwanasport
Maoni
Chapisha Maoni