Polisi aliyemkata vidole mtumishi wake afukuzwa
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limemfukuza kazi
askari wake, Sajini WP Fatuma, baada ya kuthibitika alimkata vidole vinne
mfanyakazi wake wa ndani, Steven Magesa (18).
![]()
Akizungumza mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mwanza, Valentino Mlowola, alisema baada ya kupokea taarifa za tukio la
askari huyo lililotokea Oktoba 20, mwaka huu, walichukua hatua za kiutawala na
kuanza kufanya uchunguzi.
Alisema katika hatua hizo waliunda timu maalumu ya
wachunguzi kufuatilia tukio hilo lililofanyika katika Kijiji cha Magange Mugumu
wilayani Serengeti mkoani Mara ambako ni nyumbani kwa kijana huyo na walipata
uthibitisho wa kutosha wa askari huyo kuhusika na kosa hilo hivyo kumfukuza
kazi baada ya kumsikiliza katika mahakama ya jeshi.
“Baada ya uchunguzi tulibaini kuwapo kwa udanganyifu
wa maelezo yaliyotolewa na WP Fatuma kuhusiana na tukio hilo, hivyo kutokana na
ushahidi uliowasilishwa katika Mahakama ya Jeshi, tulimtia hatiani na kuvuliwa
nyadhifa zake zote ikiwa ni pamoja na kumfukuza kazi.
“Kwa sasa WP Fatuma amesafirishwa kwenda mkoani Mara
kwa ajili ya kushitakiwa mahakamani kwa jinai. Hili ni fundisho kwa askari wetu
wengine wenye tabia kama hii na watu wengine ambao wamekuwa wakijichukulia
sheria mkononi na kufanya vitendo vya jinai kwa kushindwa kufuata sheria,”
alisema Mlowola.
Aliwataka askari kuacha kutenda makosa ya jinai,
kuwanyanyasa raia wakati wanaposhughulikia malalamiko na makosa ya jinai
yanayofikishwa katika vituo vya polisi na madawati na badala yake wazingatie
maadili na taratibu zao kutokana na wao kupewa dhamana ya kuwalinda raia na
mali zao.
Kwa upande wake, Steven, amelipongeza jeshi hilo
kutomlinda askari wake na kuamua kumchukulia hatua kali za kimaadili na
kisheria kwa kosa alilotendewa na askari huyo kwa kumtuhumu kumwibia deki ya
video na vitu vingine vya ndani vyenye thamani ya Sh 300,000 akiwa mfanyakazi
wake |
Maoni
Chapisha Maoni