Ngassa awa mfungaji bora Ligi ya Mabingwa Afrika

MSHAMBULIAJI
wa Yanga, Mrisho Ngassa amepata zali Afrika, baada ya kumaliza kinara
wa mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, licha ya klabu yake kuaga
mashindano hayo alfajiri kabisa.
Ngassa amemaliza kinara baada ya kufunga mabao
sita na kufungana na Ndombe Mubele wa AS Vita Club ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo, Haythem Jouini wa Esperance de Tunis ya Tunisia na
El Hedi Belameiri wa ES Setif ya Algeria.
Ni baada ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufikia tamati
wikiendi iliyopita na ES Setif kutangazwa mabingwa wapya wakibebwa na
bao la ugenini kutokana na matokeo ya sare bao 1-1 mchezo wa Algeria na
sare mabao 2-2 mchezo uliochezwa Kinshasa.
Ngassa aliyafunga mabao hayo katika raundi ya
kwanza walipocheza na Komorozine ya Comoro mchezo wa kwanza walishinda
7-0 na marudiano walitoka kifua mbele kwa mabao 5-2.
Yanga ilitolewa kwenye mashindano na Al Ahly ya
Misri kwa penalti 3-4. Lakini Ngassa hawezi kupewa zawadi yoyote kwavile
wamefungana na kiutaratibu hata mchezaji akishinda tuzo hiyo CAF huitoa
kwa klabu yake.-Mwanasport
Maoni
Chapisha Maoni