Mosoti: Nipo tayari kurejea Simba

BEKI wa zamani wa Simba, Mkenya Donald Mosoti amesema yupo
tayari kufuta kesi na kurejea Simba endapo tu watahitaji huduma yake na
kufikia makubaliano kimkataba.
Kauli hiyo aliitoa baada ya kuwepo na taarifa
kwamba Kocha Patrick Phiri bado anamuhitaji beki huyo wa kati katika
usajili wa dirisha dogo utakaoanza Novemba 15 ili kuboresha safu yake ya
ulinzi ambayo inaonekana kuwa tatizo ndani ya kikosi chake.
Jina la Mosoti lilikatwa siku mbili kabla ya
dirisha la usajili mpya wa Ligi Kuu Bara kufungwa ambapo nafasi yake
ilichukuliwa na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi na hivyo kuamua
kufungua kesi katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kesi ambayo
inasimamiwa na wakili wake Felix Majani kwa madai ya kuvunjiwa mkataba
wake pasipo makubaliano.
Fifa iliwataka Simba kupeleka vielelezo vyao
ikiwemo mkataba baina yao na Mosoti kwa ajili ya kuanza kusikiliza kesi
hiyo kwa pande zote mbili lakini viongozi wa Simba walishindwa kufanya
hivyo na Fifa sasa wanasubiri kutoa uamuzi wa upande mmoja.
Mosoti (pichani) aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Kesi
ipo Fifa ambao waliomba mkataba wangu na Simba ili waupitie, wakili
wangu Majani aliwapelekea hivyo kinachosubiriwa ni uamuzi tu lakini pia
kurudi Simba sio tatizo kikubwa ni kukaa na kufikia makubaliano.”
“Kama wanahitaji huduma yangu mimi sina tatizo ila
zitafuatwa taratibu na tukikubaliana kwa pamoja basi hakutakuwa na haja
ya kuendelea na kesi hivyo itafutwa,” alisema Mosoti.
Kwa sasa Simba ipo katika mikakati ya kuhakikisha
wanaimarisha kikosi chao kutokana na matokeo ya sare waliyoyapata kwenye
mechi sita za ligi.
Mabao ya Simba yote yanatokana na beki yao
kutokuwa imara kulinda lango lao pale wanapopata ushindi na kuwapa
nafasi wapinzani wao kusawazisha.
Tayari Phiri ametaja nafasi anazotaka kuzifanyia
maboresho kuwa ni straika, kiungo mkabaji, beki ya kati, beki ya kulia
na kushoto pamoja na kipa.-CHANZO Mwanasport
Maoni
Chapisha Maoni