Azam yatia maguu dili la Mkude

AZAM imeamua kuingilia kati na
kumshawishi kiungo wa Simba, Jonas Mkude aliyekuwa akinyemelewa na Yanga
atue Chamazi, Mbagala. Mchezaji amebakiza miezi sita katika mkataba
wake na Simba ambao bado hawajamuongezea ingawa tayari mazungumzo mepesi
yameanza.
Habari zilizopatikana jana Ijumaa zilieleza kwamba
viongozi wa Azam walikuwa kwenye mpango wa kumalizana na kiungo huyo
lakini hawakuweza kukamilisha mipango yao kwani Mkude yupo kambini na
timu yake nje kidogo ya mji ikijiandaa na mechi yao na Ruvu Shooting
itakayochezwa kesho Jumapili.
Baadhi ya viongozi wa Simba jana walionekana
kuhaha kuhakikisha wanafanya jitihada za kumbana mchezaji huyo ili
asisaini mkataba na Azam ambapo wao wamepanga kumalizana naye baada ya
mechi hiyo.
“Azam wamepanga kumalizana naye na wapo tayari
kwenda kumwingizia fedha kwenye akaunti yake, kinachochelewesha ni
kwamba Mkude yupo kambini lakini kuna mazungumzo ya chinichini ambayo
yamefanyika juu ya kumalizana na mchezaji huyo,” alisema mmoja wa watu
wa karibu na Mkude.
Kiongozi mmoja wa Simba alisema: “Huku (Simba)
tumefanya naye mazungumzo tu ambayo yanakwenda vizuri lakini hatujampa
mkataba tunasubiri tumalize mechi, Mkude hawezi kuondoka kwani hatua
tuliyofikia ni nzuri.”


Mapema wiki hii Mkude alionekana na gari jipya
aina ya GXMark II Grand110 ambalo inadaiwa alipewa na viongozi wake
ikiwa ni moja ya mikakati ya kumzuia ili asiondoke lakini kiongozi mmoja
wa Simba akafafanua kwamba Mkude alinunua gari hilo kwa fedha yake
ambayo alikuwa akiidai Simba.
Msimu uliopita Azam ilikuwa ni moja ya timu
iliyomtaka kwa udi na uvumba mchezaji huyo lakini alikataa kwa kuwa
mkataba wake ulikuwa bado mrefu.-Credit Mwanasport
Maoni
Chapisha Maoni