Wajumbe wataka magazeti yachapishwe kwa nukta nundu
Mwenyekiti wa kamati namba moja,Ummy Mwalimu.
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaowakilisha watu wenye ulemavu wamependekeza magazeti kuchapishwa kwa nukta nundu ili kuwawezesha kupata habari kama watu wengine.
Mwenyekiti wa kamati namba moja, Ummy Mwalimu, akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, alisema kamati hiyo kwa sasa inajadili kwa kina masuala yanayohusu maisha ya wananchi moja kwa moja.
Alisema sura ya nne Ibara ya 31 inayozungumzia uhuru wa vyombo vya habari, baadhi ya wajumbe walitaka katiba kuwabana waandishi wa habari ikiwa ni pamoja na kulinda faragha ya mtu.
Ibara ya 31(1) (a) inasema: “Kila mtu ana haki na uhuru wa kutafuta, kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa.”
Ibara ndogo wa pili inasema: “Vyombo vya habari vitakuwa huru na vitakuwa na (a) haki ya kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa wanazozipata; (b) wajibu wa: (i) kusambaza habari na taarifa kwa wananchi; na (ii) kuheshimu na kulinda utu, heshima, uhuru na staha ya wananchi dhidi ya habari na taarifa wanazozitumia, wanazozitayarisha na kuzisambaza.
Alisema wajumbe wengi walisema kifungu hicho hakijakamilika, hivyo wakapendekeza kiongezwe ili kiwabane waandishi wa habari na vyombo vya habari ili kulinda haki ya mtu na uhuru wa mtu, lakini mwisho walikubaliana kuacha lilivyoendekezwa lakini kutakuwa na maoni ya wachache.
Mwalimu alisema wajumbe wawakilishi wa watu wenye ulemavu, walitaka nyongeza kipengele cha C kisomeke taarifa zozote ziweze kuwafikia watu wenye ulemavu.
“Wajumbe tulivutana sana kuwa tutavipa vyombo vya habari mzigo mzito kwa maana ya kwamba, gazeti likichapishwa kuwe na gazeti lenye lugha ya nukta nundu...ilikuwa mjadala mkubwa. Ni mambo yaliyoleta mvutano sana. Tumewaaacha yapigiwe kura kama yaingizwe au yasiingizwe kwa kuwa yanatoa wajibu kwa vyombo vya habari,”
CHANZO:
NIPASHE
Maoni
Chapisha Maoni