TANZANIA PRISONS YATUA DAR KUIMARISHA KIKOSI CHAKE.

MAAFANDE wa Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons, ‘Wajelajela’
wanaendeleza mawindo ya ligi kuu soka Tanzania bara jijini Mbeya na sasa wanajiandaa
kucheza mechi mbalimbali za kujipima ubavu.
Kocha mkuu wa Maafande hao, David Mwamwaja amesema
vijana wake wanaendelea vizuri na mazoezi, hivyo ana imani kubwa ya kufuta
makosa ya msimu uliopita.
“Sisi tupo katika maandalizi mazuri na tunafikiria
mambo mazuri katika michezo ijayo,” alisema Mwamwaja. “Tumejiandaa barabara,
tumesajili vizuri kwa mujibu wa mapendekezo yangu. Tunajiandaa kuanza na mechi
za kirafiki dhidi ya timu ndogo kabla ya kucheza na timu kubwa”
Mwamwaja aliongeza kuwa wataanza na timu za Mbeya
ili kuona kama wameimarika na baada ya hapo watasafiri kuja jijini Dar es
salaam kwa maandalizi zaidi.
“Tunakuja kucheza mechi za kirafiki Dar es salaam,
hapo ni jiji na kuna timu nyingi za kucheza nazo.” Aliongeza Mwamwaja.
Mwamwaja aliichukua Prisons mzunguko wa pili wa
ligi kuu msimu uliopita akirithi mikoba ya Jumanne Chale.
Kocha huyo Mkongwe aliweza kuinusuru Prisons
kushuka daraja na alisubiri mpaka mechi ya mwisho dhidi ya Ashanti United
uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ili kujua hatima yake.
Katika mechi hiyo iliyokuwa inaamua ni nani kati
ya Ashanti na Prisons anabakia ligi kuu, maafande hao walishinda mabao 2 dhidi
ya kikosi cha Abdallah Kibadeni.
Maoni
Chapisha Maoni