Sekta ya Elimu yapokea Bil. 203 kutoka Benki ya Dunia

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Sifuni Mchome akifafanua jamb wakatiwa hafla fupi ya kusaini mkataba.
Serikali ya Tanzania imesaini
mkataba wa kupokea mkopo nafuu wa shilingi bilioni 203 kutoka Benki ya
Dunia kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu katika mpango wake wa
matokeo makubwa sasa(BRN).
Mkataba huo umesainiwa na Katibu
mkuu wa wizara ya fedha Dk. Servacus Likwelile huku ukiwashirikisha
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elinu na Naibu Katibu Mkuu kutoka TAMISEMI leo
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo
fupi ya kusaini mkataba Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk. Servacus
Likwelile ameishukuru Benki ya Dunia kutoa mchango huo kusaidia sekta ya
elimu nchini na kuwataka TAMISEMI na Wizara ya Elimu kusimamia vizuri
pesa hizo ili kuleta mafanikio zaidi kufikia malengo ya matokeo makubwa
sasa.
Aidha Dk. Likwelile amewataka
waajiri wote katika sekta ya elimu kutoa kipaumbele kwa walimu ili
waweze kuboresha elimu nchini na kuwataka kupeleka majina na akaunti
namba za walimu wote Hazina ili Hazina iweze kuwawekea mishahara yao
katika akaunti zao kwa wakati.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu
Prof. Sifuni Mchome amesema kuwa Wizara ya Elimu kwa sasa imepiga hatua
kubwa katika kufanikisha lengo la matokeo makubwa sasa linalolenga
kukuza na kuendeleza elimu katika ngazi ya shule za msingi na sekondari
hivyo fedha hizo zinatumika kutatua matatizo katika sekta ya elimu
ambapo kwa sasa shule nyingi zimeanza kuonesha matokeo mazuri.
Akitoa mchango wake wakati wa
hafla hiyo Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Uganda na
Burundi Bw. Philippe Dongier amesema kuwa Benki ya Dunia imeona kuna
umuhimu wa kuisaidia Tanzania katika sekta ya elimu ili kuleta ujuzi na
kuvumbua vipaji kwa vijana wadogo watakaosaidia kuleta maendeleo hapo
baadae.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI
Dk. Deo Mtasiwa ameahidi kusimamia fedha hizo kwa ufanisi na
kuhakikisha kuwa zinawafikia walengwa wote hadi ngazi ya chini waweze
kufaidika na pesa hizo.
Maoni
Chapisha Maoni