Maporomoko ya ardhi yaua watu 32

Maporomoko ya ardhi Japan
Watu wapatao 32 wameuawa katika maporomoko ya ardhi katika mkoa wa Hiroshima nchini Japan.
Maporomoko ya ardhi yametokea katika eneo la makaazi ya watu karibu na mlima katika vitongoji vya mji wa Hiroshima.Maporomoko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zilizonyesha kwa saa 24 kuamkia Jumatano asubuhi zikiwa sawa na kipimo cha mvua za mwezi mzima, limesema Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japan.
Picha kutoka eneo la tukio zimeonyesha nyumba zikiwa zimefukiwa katika matope na miamba, wakati kikosi cha uokoaji kikielekea nyumba hizo.
Watu wengine tisa bado hawajulikani walipo, limesema shirika hilo.
Afisa mwingine wa serikali ya mtaa katika mji huo amesema "baadhi ya watu wamechukuliwa na maji na ilikuwa vigumu kujua kwa uhakika idadi yao", Shirika la habari la AP limesema.
Mwandishi wa habari wa BBC Rupert Wingfield-Hayes amesema wengi wa waliokufa ni watoto.
Mmoja mwenye umri mdogo kabisa kufariki dunia katika tukio hilo ni mvulana mwenye umri wa miaka miwili, Shirika la habari la Japan, Kyodo limeripoti.
Miongoni mwa waliokufa ni mfanyakazi wa uokoaji mwenye umri wa miaka 53 ambaye amekufa baada ya udongo kuporomoka tena, shirika la Hali ya Hewa la Japan limesema. Aliweza kuwaokoa watu watano wakati wa operesheni hiyo.
Maoni
Chapisha Maoni