Machumu mshindi tuzo uongozi Afrika Mashariki

Nairobi. Kampuni inayofanya utafiti wa Utawala Bora katika nchi
za Afrika ya CEO Titans Building Nations ya Afrika Kusini, imemtunuku
tuzo mbili Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited
(MCL), Bakari Machumu.
Kampuni ya Mwananchi ndiyo inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizens.
Machumu alipata Tuzo ya Uongozi Thabiti katika Vyombo vya Habari vya Tanzania, pia Afrika Mashariki.
Upande mwingine, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi nchini, Titus Kamani naye alikabidhiwa Tuzo ya Utawala Bora katika
kipengele cha Watendakazi Bora wa Serikalini wa Afrika.
Machumu na Waziri Kamani walikabidhiwa tuzo hizo juzi usiku katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Hilton jijini Nairobi, Kenya.
Kampuni CEO Titans Building Nations inajihusisha
na kutambua watu wanaofanya kazi kwa juhudi kwa ajili ya maendeleo ya
mataifa yao, hata kuthubutu kuvuka mipaka katika utekelezaji wa majukumu
yao.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Machumu
alisema kuwa amefurahi na ni fahari kubwa kuona kazi yake na taaluma ya
habari kwa jumla vikithaminiwa.
“Vyombo vya habari vina jukumu la kuleta
mabadiliko katika jamii. Viongozi wa nchi za Afrika wanatakiwa kufahamu
mchango wa vyombo vya habari na kushirikiana navyo katika kufikisha
habari kwa jamii,” alisema na kuongeza:
“Viongozi wa nchi za Afrika na Tanzania kwa jumla,
wanatakiwa kuruhusu watu kuzungumza mambo kwa uwazi na wasifanye vyombo
vya habari kuwa ni maadui, bali washirikiane navyo katika kuleta
maendeleo.”
Naye Waziri Dk Kamani alisema amefurahia tuzo hiyo
na kwamba inaonyesha jinsi wizara yake inavyofanya kazi kwa usahihi na
kutambulika hata nje ya mipaka ya Tanzania.
“Nimeshangaa kuona kazi ya wizara yangu
imetambuliwa namna hii. Tuzo hii si yangu pekee, bali ni ya wafanyakazi
wote wa wizara, pia Watanzania kwa jumla,” alisema.
Waziri huyo alitoa wito kwa viongozi wa Afrika wajitahidi kuwatumikia watu wote ili kusukuma mbele maendeleo.-Chanzo Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni