Logarusic aondoka kwa mkwara Simba

ALIYEKUWA Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic ameondoka nchini
usiku wa kuamkia jana Jumatano akiwa na siri kubwa moyoni huku
akiwaambia Wanasimba ‘Mtanikumbuka’.
Logarusic ambaye alikuwa kimya tangu
alipositishiwa mkataba wake wikiendi iliyopita, alifanya mahojiano na
Mwanaspoti dakika chache kabla ya kupanda ndege kurejea kwao Croatia
huku akiwa makini na kusisitiza atakumbukwa.
Akizungumza Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere,
Logarusic alisema: “Sina tatizo lolote na nashukuru kwa kuachishwa kazi
maana ukiwa kocha hivi ni vitu vya kawaida kutokea. Kuhusu sababu za
kutimuliwa kwangu, naona ni siasa tu ndiyo iliyotumika hakuna jipya,
kosa langu ni kutokubali kuwa mwanasiasa katika soka.
“I came as a man, I act as a coach and I leave as a
gentleman (Nilikuja kama mtu, nikaishi kama kocha na naondoka
mwanaume), wanachama na mashabiki wa Simba watanikumbuka siku si nyingi
kwa mambo niliyokuwa nayaandaa kwao na hata niliyofanya.”
Logarusic alisema sababu nyingi zilizoelezwa
kuhusu kutimuliwa kwake, ni za kuhalalisha yeye kuondoka kwani hakuwa
tayari hata kidogo kuona siasa inaingilia kazi yake.
“Naiacha Simba ikiwa na kikosi cha ubingwa, ndiyo
kikosi hiki kinaweza kutwaa ubingwa na kama ningebaki nacho hakika
ningechukua ubingwa. Najua kocha mpya atakuja lakini muda si mrefu
wanachama wataujua ukweli na hapo ndipo nitakapokumbukwa,” alisema
Logarusic.
Kuhusu tabia ya ukali kwa wachezaji, Logarusic
alisema: “Nilikuwepo tangu mwanzo wa mwaka chini ya uongozi mwingine,
sasa leo hii ndiyo naonekana mkali? Inawezekana lakini nilikuwa
natekeleza majukumu yangu.
“Mimi ni binadamu hata hizo tabia zangu nje ya
uwanja, ni mambo yangu binafsi hivi tukiangaliana mmoja mmoja ni nani
aliyetimia? Sisi ni binadamu tuhukumu ambayo hata sisi hatuwezi
kufanya.”
Logarusic ambaye amewahi kuzifundisha Hearts of
Hoek ya Ghana na Gor Mahia ya Kenya, alijiunga na Simba Desemba mwaka
jana na kuingoza katika mechi 21, kati hizo ameshinda nane, amefungwa
nane na kutoka sare tano.-mwanasport
Maoni
Chapisha Maoni