Serikali kusambaza vipimo vya ebola

Akuzungumzia azma hiyo, Naibu Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe alisema kuwa mashine hizo zitasaidia
kubaini maambukizi ya virusi vya ebola kwa haraka katika viwanja vya
ndege bila kuathiri safari za abiria.
Dk. Kebwe ambaye alikuwa Afrika Kusini kuhudhuria
kikao cha dharula cha nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa
Afrika (Sadc), alisema katika kikao hicho walikubaliana kuchukua
tahadhari kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo mengine barani
Afrika.
Aliongeza kuwa mashine za kupima joto zitasambazwa
katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (JNIA), Kilimanjaro (KIA),
Arusha, Zanzibar na Mbeya.
Alisisitiza kuwa bado taifa lina vifaa vya kutosha
vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ebola, endapo ugonjwa huo
ukifika nchini.
“Niwahakikishie Watanzania kuwa hakuna mtu
atakayekufa kwa ugonjwa wa ebola kwa sababu ya kukosa huduma. Hakuna
haja ya kuwa na hofu, Serikali tumejipanga kikamilifu kuzuia ugonjwa huu
wakati wote,” alisema.
Aprili 2013, Serikali ilipokea msaada wa vifaa
maalumu vya kuzuia maambukizi ya virusi vya ebola kutoka Serikali ya
Marekani kupitia mpango wake wa USAID. Msaada huo unajumuisha makasha
320 yenye vifaa vya kutosha watumishi wa afya 16,000.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD),
Cosmas Mwaifwani alibainisha kuwa vifaa vilivyomo katika makasha ni
pamoja na magauni maalumu yanayovaliwa na wahudumu wa afya ili kuwakinga
kugusana na wagonjwa na vitambaa maalumu wanachovaa wahudumu juu ya
gauni hilo.
Vifaa vingine ni miwani maalumu inayokinga macho,
glovu maalumu zinazovaliwa mikononi na kitambaa maalumu chenye dawa
ambacho kinatumika kujisafisha endapo mtumishi atapata jeraha lolote
wakati akitoa huduma.
Maoni
Chapisha Maoni